Na: Asifiwe Mbembela
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kupitia Mradi wa
Tathmini ya Mapato ya Kaboni kama Njia Endelevu ya Uwezeshaji Kifedha katika
Uhifadhi na Usimamizi wa Misitu ya Jamii Tanzania kimewajengea uwezo maafisa na
wananchi kutoka maeneo yenye hifadhi za misitu ya vijiji pamoja na baadhi ya
vijiji vyenye misitu ya hifadhi za vijiji ambao wanashiriki biashara ya kaboni
na wemeshapata mapato yanayotokana na biashara hiyo.
Wakizungumza wakati wa mafunzo hayo, wananchi wa vijiji ambavyo
havijaanza kunufaika na mapato ya kaboni akiwemo Bw. Mwanangao Msanya kutoka
Mvomero mkoani Morogoro amesema wamekuwa wakihifadhi misitu ya Kijiji kwa muda
sasa lakini mafunzo hayo yamewapa uelewa mpya wa vigezo na taratibu za kuingia
na kunufaika na biashara ya kaboni.
Afisa Misitu Mwandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Siima Bakengesa akifungua warsha hiyo iliyohusisha wadau kutoka asasi za kiserikali na asasi zisizo za kiserikali na baadhi ya wananchi wa Wilaya za Tanganyika, Mbulu, Mvomero, Mwanga na Korogwe, amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuimarisha uhifadhi wa bioanuwai na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia usimamizi shirikishi wa misitu ya vijiji.
Mtafiti Kiongozi wa Mradi, Dkt. Kajenje Nkukurah amesema SUA
inaamini mafunzo hayo yatawezesha vijiji ambavyo bado havijaingia katika
biashara ya kaboni kufanya maamuzi sahihi kuhusu ushiriki wao pamoja na
kuimarisha utawala na usimamizi wa mapato katika ngazi ya vijiji.
Ameongeza kuwa mradi unalenga kuwajengea uwezo wananchi wa vijiji vyenye misitu iliyo katika biashara ya kaboni ili waweze kuendelea kunufaika kiuchumi kupitia biashara ya kaboni, huku mapato yakitumika katika usimamizi endelevu wa misitu ya hifadhi ya vijiji na kuchochea maendeleo endelevu.
Akitoa ushuhuda wakati wa kuwasilisha sauti za jamii, Afisa Misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Bw. Bruno Mwaisaka amesema wilaya hiyo imepokea zaidi ya shilingi bilioni 34 kutokana na biashara ya kaboni ambapo fedha hizo zimechangia kuboresha ustawi wa jamii kupitia ujenzi wa shule, vituo vya afya na kutoa ajira za muda kwa wananchi huku pia zikiongeza ari ya jamii kushiriki katika uhifadhi na usimamizi wa misitu.
Kwa upande wake, Dkt. Neal Hockley, Mtafiti, na Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Bangor nchini Uingereza amesema katika kutathmini biashara ya kaboni, wananchi wanapaswa kuangalia kwa kina faida na gharama zake kwa kulinganisha na shughuli nyingine za kiuchumi, ikiwemo kilimo.
Mradi wa Tathmini ya Mapato ya Kaboni kama Njia Endelevu ya
Uwezeshaji Kifedha katika Uhifadhi na Usimamizi wa Misitu ya Jamii Tanzania ni
wa miaka mitatu unaotekelezwa na SUA kama taasisi inayoongoza, kwa kushirikiana
na NCMC na Chuo Kikuu cha Bangor cha Uingereza ukifadhiliwa na Defra
kupitia GCBC, DAI, ISPF pamoja na Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali
ya Uingereza.



.jpg)


0 Comments