Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, aliyemwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amepongeza ushirikiano wa kimkakati kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), pamoja na Chuo Kikuu cha Simon Fraser Canada katika kuendeleza utafiti, ubunifu na matumizi ya maarifa kwa maendeleo ya jamii.
Mhe. Wanu alitoa pongezi hizo tarehe 23 Septemba 2026 wakati wa Kongamano la Tatu, lililofanyika katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Arusha. Kongamano hilo linawakutanisha wadau kutoka taasisi hizo kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano, kubadilishana maarifa na kujadili suluhisho bunifu za changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii. Kongamano lililopita lilifanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro, mwaka 2025.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mhe. Wanu alisisitiza umuhimu wa kutumia uchambuzi wa takwimu, sayansi, teknolojia na ubunifu katika kukabiliana na changamoto za kijamii, kuimarisha elimu ya juu na kuchochea maendeleo katika sekta za afya, kilimo na mazingira.
Aidha, Mhe. Wanu alitoa wito kwa watafiti na taasisi za elimu ya juu kuhakikisha matokeo ya tafiti na maarifa yanayozalishwa kupitia ushirikiano huo yanatafsiriwa kuwa suluhisho za vitendo zenye tija na zinazoboresha maisha na ustawi wa Watanzania.
Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuongeza jitihada za utafiti kuhusu mabadiliko ya tabianchi na athari zake katika uzalishaji, hususan katika sekta ya kilimo, huku akihimiza matumizi ya matokeo ya tafiti katika kujenga uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuendeleza maendeleo endelevu.
.jpg)

.jpg)

0 Comments