Na: Farida Mkongwe
SUA
Media imeendelea kujipambanua katika tasnia ya habari baada ya kutunukiwa tuzo
maalum ya ushiriki katika Kongamano la Tano la Idhaa za Kiswahili Duniani
lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa
(BAKITA).
Tuzo hiyo iliyotolewa jijini Arusha Machi 26, 2026 inaakisi utambuzi wa mchango mkubwa wa vyombo vya habari, ikiwemo SUA Media, katika kutoa elimu kwa jamii na kuhamasisha matumizi sahihi ya lugha adhimu ya Kiswahili
Akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Mhadhiri Mwandamizi Dkt. Onesmo Nyinondi, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Taaluma za Lugha, ameipongeza SUA Media kwa mafanikio hayo.
“SUA tukiendelea kushiriki kwenye majukwaa kama
haya tunazidi kuonekana na kuijulisha dunia kuwa SUA siyo kwa ajili ya kilimo
na zile sayansi ngumu pekee, bali hata sayansi hizo zinaweza kumfikia mlaji kwa
lugha adhimu ya Kiswahili,” amesema Dkt. Nyinondi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Nyinondi amewataka watangazaji wa SUA Media, hususan vijana, kuendelea kujinoa katika matumizi ya lugha ya Kiswahili na kuepuka kuchanganya lugha wanapowasilisha vipindi.
Aidha, ametoa wito kwa watangazaji kushiriki mafunzo ya umahiri wa Kiswahili ili kuongeza ubora wa mawasiliano na kuweza kutangaza kwa ufasaha shughuli mbalimbali zinazofanywa na chuo, hatua itakayosaidia kuongeza ushawishi na hadhi ya SUA katika tasnia ya habari.Kongamano hilo limewakutanisha wadau mbalimbali wa tasnia ya habari, wakiwemo watangazaji wa redio, blogu, wahariri, maofisa habari, pamoja na wanafunzi wa utangazaji na vituo vya televisheni vinavyotangaza kwa lugha ya Kiswahili duniani, ambapo washiriki wote walipewa vyeti.






0 Comments