Na: Farida Mkongwe
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, amesema Serikali
imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya kukuza na kuendeleza matumizi ya lugha
ya Kiswahili kupitia fursa mbalimbali zikiwemo ukalimani, tafsiri, uhariri,
uandishi, utangazaji wa habari na ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni kwa lengo
la kuiwezesha lugha ya Kiswahili kuwa chombo muhimu cha ajira na uchumi kwa watanzania.
Akizungumza jijini Arusha Machi 24, 2026, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Tano la Idhaa za Kiswahili Duniani lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), Mhe. Makonda amesema Serikali imefanikiwa kupanua wigo wa ufundishaji wa Kiswahili kwa kufungua vituo 20 nje ya nchi kupitia balozi za Tanzania na vituo 35 ndani ya nchi, idadi ambayo imeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka vituo viwili vya nje ya nchi na vitatu vya ndani vilivyokuwepo miaka mitano iliyopita.
Aidha, Waziri Makonda amesema Tanzania inaendelea kuwa kinara katika kukuza Kiswahili kimataifa, ikiwa ni nchi pekee iliyofanikiwa kufungua vituo vya ufundishaji wa Kiswahili nje ya mipaka yake.
“Wizara
yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo
Zanzibar pamoja na mabaraza ya Kiswahili ya BAKITA na BAKIZA, itaendelea
kutekeleza mikakati ya kukuza lugha hiyo ili iende sambamba na maendeleo ya
dunia ya sasa”, amesema
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, akifungua kongamano hilo, amewahimiza Watanzania kuendelea kudumisha amani na mshikamano, akisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo ya taifa.
Mhe. Hemed
amesema kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa, huku akiwataka
wananchi kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ili kwa pamoja taifa liweze
kufikia malengo ya maendeleo yaliyokusudiwa.
Kongamano
hilo, lenye kauli mbiu isemayo “Tasnia ya Habari, Msingi wa Maendeleo ya
Kiswahili Duniani”, limeandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na
limewakutanisha wadau wa Kiswahili kutoka ndani na nje ya nchi.
Miongoni
mwa washiriki wa kongamano hilo ni pamoja na SUA Media, ambao wameendelea
kushiriki kikamilifu katika kuhabarisha na kuelimisha umma kuhusu mchango wa
Kiswahili katika maendeleo ya jamii.
.jpeg)
.jpeg)





0 Comments