Na: Ayoub Mwigune
Watafiti, wahadhiri na
wanafunzi wa Shahada za Uzamili na Uzamivu wametakiwa kuzingatia uandishi wa
machapisho ya kisayansi yenye ubora wa kimataifa, ili kuongeza tija katika
tafiti na kuimarisha heshima ya vyuo vikuu vya Afrika kwenye majukwaa ya kitaaluma
ya kimataifa.
Hayo yameelezwa katika mjadala wa kitaaluma ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa NANO COM, uliolenga kuboresha uelewa wa uandishi wa kisayansi na ubora wa machapisho.
Awali, Prof. Gaymary Bakari,
ambaye ni Kiongozi wa Mradi wa NANO COM nchini Tanzania na Naibu Rasi wa Ndaki
ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya (SUA), amesema kuwa uandishi wa kisayansi
ni ujuzi muhimu kwa kila mwanafunzi na mtafiti, kwani ndio kipimo cha kazi ya
kitaaluma duniani.
“Kupitia mradi wa NANO COM,
tunalenga kuwajengea uwezo watafiti na wanataaluma wetu ili waandike machapisho
yenye ubora unaokubalika kimataifa. Hii itasaidia kuongeza machapisho kutoka
SUA na vyuo vikuu vingine nchini,” amesema Prof. Gaymary.
Akichangia katika mjadala huo, Prof. Xin Zhao kutoka Chuo Kikuu cha McGill , Canada, amesisitiza kwamba ubora wa elimu na utafiti wa kisayansi ndio unaoamua maendeleo ya taifa. Amesema nchi zilizoendelea zimefanikiwa kwa sababu zimewekeza katika elimu, tafiti, na mfumo wa kuchapisha matokeo ya kisayansi kwa uwazi.
“Katika nchi nyingi
zilizoendelea, wanafunzi hawawezi kuhitimu bila kuchapisha makala kwenye
majarida yenye viwango vya juu, na wanasayansi hupandishwa vyeo kwa kuzingatia
machapisho yao,” amesema Prof. Zhao.
Prof. Zhao pia ametoa ushauri
kwa wanataaluma na wanafunzi wanaoanza safari ya utafiti, akisisitiza kuelewa
uzito na mchango wa tafiti zao kwa jamii sambamba na kuepuka kurudia tafiti
zilizofanywa tayari na kufanya tafiti zenye ubunifu na mchango mpya katika
jamii.
0 Comments