SUAMEDIA

SUA yatunuku Shahada kwa wahitimu 3,560, yawahimiza ubunifu na uzalendo

 Na: Farida Mkongwe

Jumla ya wahitimu 3,560 kutoka programu 85 za masomo ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wametunukiwa Shahada mbalimbali za Chuo hicho, kati yao, wanaume ni 2,029 na wanawake 1,531, sawa na asilimia 43 ya wahitimu wote.

Akitoa takwimu hizo Oktoba 16, 2025 kwenye Mahafali ya 46 ya Chuo hicho, Makamu wa Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda, amesema wahitimu wa Shahada za Kwanza wapo 3,274kati yao wanaume 1,861 na wanawake 1,413, Shahada za Umahiri wahitimu 127, wanaume 76 na wanawake 51.

Wahitimu wa Shahada ya Uzamivu ni 18 kati yao wanaume 12 na wanawake 6, wahitimu wa Stashahada wakiwa 100, wanaume 53 na wanawake 47 na wahitimu wa Astashahada 38 ambapo wanaume ni  26 na wanawake 12.

Prof. Chibunda amewapongeza wahitimu kwa juhudi na bidii waliyoonesha katika masomo yao, “Kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo haijawahi kuwa lelemama, kwa dhati kabisa ya moyo wangu ninayo furaha kubwa kuwapongeza wahitimu wote ambao utawatunuku shahada zao katika mahafali haya, hongereni sana.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Mhe. Andrew Massawe, amewapongeza wahitimu kwa juhudi na nidhamu waliyoonesha. “Leo ni siku ya kihistoria katika maisha yenu, mmeonesha ujasiri, bidii na kujituma, hongereni sana kwa mafanikio haya,” amesema Mhe. Massawe.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Chuo amewataka wahitimu kutumia maarifa waliyopata SUA kwa ubunifu, ujasiriamali na uzalendo, akisisitiza kuwa dunia ya sasa inahitaji vijana wabunifu na wanaotumia teknolojia kama nyenzo ya maendeleo, “Msiogope kujaribu mambo mapya, tumieni elimu yenu kubuni suluhisho la changamoto za jamii, kujiajiri na kuajiri wengine,” amesisitiza.

Aidha, Mhe. Massawe amebainisha kuwa Baraza la Chuo limeendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, uadilifu na uzalendo, likiwa na lengo kuu la kuhakikisha kwamba SUA inaendelea kuwa taasisi mahiri ya elimu ya juu, utafiti na utoaji wa huduma bora kwa jamii.

Baadhi ya wahitimu, akiwemo Creva Nyitwike Nyabare,  Christine Mbaga na Happness Ngimbile wamesema safari ya masomo haikuwa rahisi lakini wamepambana na kufanikisha na kwamba watatumia  elimu waliyoipata kwa manufaa ya jamii na kuhimiza wanafunzi wengine kujiunga na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo chenye walimu bora na mafunzo yanayowawezesha kupata ajira au kujiajiri.







Post a Comment

0 Comments