SUAMEDIA

SUA yashirikiana na Ashish Life Science kuwatambua wanafunzi bora wa tiba ya wanyama

 Na: Farida Mkongwe

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kupitia Ndaki ya Tiba ya Mifugo na Sayansi za Afya, kimewatambua na kuwatunuku zawadi wanafunzi waliopata ufaulu wa juu katika masomo yao ya tiba ya wanyama, tukio ambalo limefanyika Oktoba 15, 2025, kwa ushirikiano na kampuni ya kimataifa ya dawa za mifugo, Ashish Life Science (ALS), ambayo imekuwa mshirika mkubwa wa SUA kwa miaka mitano mfululizo katika kuinua ubora wa elimu ya tiba ya mifugo nchini.


Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Ezron Karimuribo, Rasi wa Ndaki ya Tiba ya Mifugo na Sayansi za Afya, amesema ushirikiano huo kati ya SUA na ALS umekuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi, “Kampuni hii imekuwa ikiwatia moyo vijana wetu kwa kuwapatia elimu kuhusu dawa mpya sokoni, kutoa ajira kwa wahitimu wetu, na kuanzisha programu za mafunzo kwa vitendo (internship) zinazowaandaa wanafunzi kwa maisha ya kitaaluma,” amesema Prof. Karimuribo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ALS Tanzania, Dkt. Sanjeev Sarkar, amesema kampuni hiyo yenye makao makuu nchini India imejikita katika kuhakikisha afya, ustawi, na uzalishaji bora wa wanyama duniani huku akisisitiza kwamba ushirikiano wake na SUA umeendelea kuwa chachu ya kukuza wataalamu wabunifu na wenye ujuzi katika sekta ya mifugo, hivyo kuchangia moja kwa moja katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania kupitia afya bora na uzalishaji wa mifugo.

“Tumekuwa tukitoa nafasi ya mafunzo kwa vitendo (internship) kila mwaka kwa wanafunzi wa SUA, mwaka huu, nafasi hiyo imekwenda kwa Issa Mpogo, mhitimu wa mwaka wa tano wa Shahada ya Tiba ya Wanyama, ambaye atapata fursa ya kujifunza na kuboresha uwezo wake katika kutoa huduma za tiba kwa wanyama,” amesema Dkt. Sarkar.

Wakizungumza katika hafla hiyo, baadhi ya wahitimu waliotunukiwa zawadi, akiwemo Martina Charles Mgeni, wameeleza kwamba tuzo hiyo ni heshima kubwa na motisha ya kuendelea kufanya vizuri zaidi, “Ni furaha kwangu kuona chuo kimetambua juhudi zangu kwani hii inanipa hamasa zaidi kuendelea kufanya vizuri katika taaluma ya tiba ya wanyama,” amesema Martina kwa furaha.

Kwa upande wake Issa Mpogo, aliyeshinda tuzo na pia kupata nafasi ya mafunzo kwa vitendo katika ALS, amesema: “Kupitia internship hii nitajifunza mbinu bora zaidi za tiba, matumizi salama ya dawa, na nitachangia maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.”

Katika hafla hiyo, kampuni ya ALS ilitoa zawadi kwa wanafunzi watano bora zaidi katika nyanja mbalimbali, huku pia wanafunzi wa ngazi ya diploma waliosaidia madaktari wa wanyama wakitambuliwa kwa mchango wao mkubwa katika kuboresha huduma za tiba ya mifugo nchini.









 

Post a Comment

0 Comments