SUAMEDIA

SUA yapongezwa kwa mageuzi ya mitaala yanayoendana na mahitaji ya dunia ya sasa

 Na: Farida Mkongwe

Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam kutoka Chuo cha Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam, Prof. Sotco Komba, amepongeza hatua kubwa zinazochukuliwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika kuboresha mitaala yake ili iendane na mabadiliko ya dunia ya sasa na mahitaji ya soko la ajira.

Akizungumza katika mkutano wa mwaka wa SUA CEO Alumni Forum 2025, uliowakutanisha wahitimu na watumishi waliowahi kusoma au kufanya kazi chuoni hapo ambao kwa sasa ni wakurugenzi na watendaji wa taasisi mbalimbali, Prof. Komba amesema SUA imeonesha dira na ubunifu mkubwa katika kuhakikisha elimu inayotolewa inazalisha wataalamu wabunifu, wenye uwezo wa kujiajiri na kuajirika.

Amesema kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa sasa, alikuwa Mhadhiri SUA, hivyo anaifahamu vizuri safari ya mageuzi ya kitaaluma ya chuo hicho, “Leo tumefurahia sana kurudi nyumbani SUA, tumeona miradi mingi ya kimkakati ikiwemo shamba la mfano na kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa za nguo, ambavyo vinaonesha kwa vitendo falsafa ya elimu inayochanganya nadharia na vitendo,” amesema Prof. Komba.

Ameongeza kuwa miongoni mwa mambo yaliyomvutia ni maboresho ya mitaala mipya ambayo yanajikita katika kumjengea mwanafunzi stadi muhimu za maisha na kazi, “Mitaala hii inaakisi mwenendo wa dunia wa sasa, inamwezesha mwanafunzi sio tu kupata maarifa ya kitaaluma, bali pia kujifunza ujuzi wa kujiajiri na kutatua changamoto za jamii,” amesema Prof. Komba.

Prof. Komba amesema ana imani kuwa kupitia mageuzi hayo, SUA itaendelea kuwa taasisi imara na kinara wa elimu ya ubunifu nchini, “Kwa hakika, tunajivunia kuona SUA ikiendelea kuwa mfano wa ubora wa elimu, ubunifu na mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii ya Watanzania,” amesisitiza.







Post a Comment

0 Comments