Na: Gerald Lwomile
Serikali imesema elimu ya kilimo
ni nguzo muhimu katika kukabiliana na changamoto za usalama wa chakula,
mabadiliko ya tabianchi, na ajira kwa vijana.
![]() |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli (kushoto) akikabidhi zawadi |
Akizungumza katika hafla ya
Majalisi ya 42 ya ugawaji tuzo kwa wanafunzi na watumishi waliofanya vyema
kitaaluma, utafiti na ubunifu katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Katibu
Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli amesema utaratibu huo ni ishara ya safari ndefu ya umahiri,
ubunifu, na kujituma inayokipambanua chuo hicho.
Amesema chini ya uongozi wa
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, serikali imeendelea kuwekeza katika program
mbalimbali za kuwajengea vijana uwezo katika kilimo kama BBT, SUA STEPS na Mpango wa Kukuza na Kuendeleza Kilimo Biashara AIP, ambazo
zinawawezesha vijana kujiajiri na kuwa wabunifu katika mnyororo wa thamani wa
kilimo.
“Elimu, hasa katika fani ya
kilimo, lazima ishughulikie mahitaji halisi ya jamii yetu. Kutokana na
changamoto zinazojitokeza katika eneo la usalama wa chakula, mabadiliko ya
tabianchi, na ukosefu wa ajira vijijini, Taasisi kama Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo zimekuwa muhimu zaidi kuliko hapo awali” amesema Mweli.
Amesema SUA ina wajibu mkubwa si
tu kwa Tanzania bali pia kwa bara la Afrika katika kutoa wahitimu na watafiti
watakaosaidia katika uzalishaji wa chakula ili kukabiliana na ukosefu wa
chakula na kuboresha mifumo ya chakula duniani.
Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu
wa Wizara ya Kilimo Bw. Mweli ameipongeza SUA kwa kupitia upya mitaala yake ili
iendane na mahitaji ya soko la ajira la karne ya 21.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika
Majalisi hayo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael
Chibunda amesema zaidi ya vijana na wanataaluma 180 wamefanya vizuri katika
masomo, utafiti na ubunifu mbalimbali na wanapata zawadi kuanzia shilingi elfu
50 hadi milioni moja.
Prof. Chibunda amewapongeza
wahitimu wote waliofanya vizuri katika masomo yao na kuwa ana matumaini makubwa
wataenda kufanya vizuri kila wanapokwenda na katatua changamoto mbalimbali
katika jamii inayowazunguka.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Prof. Maulid Mwatawala amesema utaratibu huo wa kawaida wa chuo kutoa zawadi kwa wanafunzi na wanataaluma waliofanya vyema katika masomo na tafiti ni kichocheo cha kuongeza ufanisi katika masomo, utafiti na ubunifu.
0 Comments