SUAMEDIA

SUA yapata miradi mipya 36 ya utafiti yenye thamani ya sh. bilioni 10.5

 Na: Farida Mkongwe

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimefanikiwa kupata miradi mipya ya utafiti 36 yenye thamani ya Shilingi bilioni 10.5, inayolenga kufanya tafiti zinazoongeza maarifa na kutatua changamoto katika sekta za kilimo, mifugo, mazingira na maendeleo ya jamii.


Akizungumza wakati wa Mahafali ya 46 ya chuo hicho yaliyofanyika katika Kampasi ya Edward Moringe, Morogoro, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Mhe. Andrew Massawe, amesema miongoni mwa miradi hiyo, miradi 10 inafadhiliwa na wafadhili wa nje, miwili na Serikali kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), huku miradi 24 ikifadhiliwa na SUA kupitia mapato yake ya ndani.

“Tangu Mahafali ya 45 yaliyofanyika Mei 22, 2025, Baraza limefanikisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali zilizolenga kuboresha utendaji wa Chuo katika maeneo tofauti, likiwa na lengo kuu la kuhakikisha SUA inaendelea kuwa taasisi mahiri ya elimu ya juu, utafiti na utoaji wa huduma bora kwa jamii,” amesema Mhe. Massawe.

Aidha, amesema pamoja na mafanikio hayo, Baraza la Chuo linaendelea kuimarisha vyanzo mbadala vya mapato kupitia miradi ya kibiashara, utoaji wa ushauri wa kitaaluma na uwekezaji katika maeneo ya kimkakati, sambamba na kuhimiza matumizi ya matokeo ya tafiti katika sera na mipango ya maendeleo ya taifa.

 


 


Post a Comment

0 Comments