SUAMEDIA

SUA imeenda na kasi ya mabadiliko ya Sera ya Elimu - TCU

Na Josephine Mallango

Mkurugenzi wa Ithibati kutoka  Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Dkt. Telemu Kassile  amekipongeza  Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuendana na kasi ya mabadiliko ya Sera mpya ya Elimu ya 2023 inayosisitiza mitaala ya sasa ambayo itawapa wahitimu ujuzi wa kuweza kuajiriwa au kujiari  popote watakapokuwa mara baada ya kuhitimu masomo yao.  

Akifungua warsha Mkoani Morogoro Dkt. Kassile amesema  SUA wameandaa  mafunzo ya siku 5 ya  kuwajengea uwezo wanataaluma na viongozi mbalimbali katika ngazi tofauti tofauti  SUA mara baada ya  kuhuisha mitaala yake, na kutengeneza mitaala mipya  iliyozingatia hali halisi.

"Pongezi SUA, wanaenda na kasi ya mabadiliko Mafunzo haya yanalenga zaidi katika kuwapa mbinu washiriki ya namna ya kufundisha mitaala iliyofanyiwa marejeo baada ya sera ya elimu na  mafunzo ya mwaka  2014 kufanyiwa mapitio na kutolewa toleo la mwaka 2023 kwa kuwa sera hiyo imesisitiza  zaidi wahitimu kuweza kuwa na na ujuzi na sisi TCU kama wasimamizi tulitoa maelekezo kwa  vyuo vikuu vyote nchini kuhuisha mitaala yao na wanaoandaa mitaala mipya waweze kuandaa mitaala ambayo itawapa  wahitimu ujuzi wa kuweza kuajiriwa au kujiari” amesema Kassile.


Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo upande wa Taaluma , Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Prof. Maulid Mwatawala amesema, wanafunzi wa SUA  watanufaika na utekelezaji wa  mabadiliko ya sera kwa kuboresha kuanzia utoaji wa mafunzo ambao kwa sasa utabadilika kwa kuongeza  watu  wanaotoka kwenye  viwanda na sehemu zingine za kazi ambao wanauzoefu na siyo waalimu wa SUA pekee ambao watakuja na stadi walizonazo na ufundishaji sambamba na ufundishaji wa kidigi.

Ameongeza kuwa Sehemu kubwa ya mafunzo kwa sasa  mwanafunzi ataweza kujifunza wenyewe na kushirikiana na wenzake tofauti na mfumo wa zamani ambao mwalimu alisimama mbele na kufundisha  kile anachojua sanjari na mabadiliko katika  mfumo wa mafunzo kwa vitendo ambapo kwa sasa  mwanafunzi  mwaka wa mwisho atakaa sehemu ya mafunzo ya vitendo kwa semista nzima ili ajifunze  stadi za kazi na mazingira ya kazi ili akimaliza anakuwa tayari kuanza kazi  tofauti na mfumo wa  zamani  mwanafunzi alikuwa  anaenda mafunzo kwa vitendo kwa  wiki 5.

Nae Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango , Utawala na fedha Prof. Amandus Muhairwa amesema katika mafunzo haya wanawataka wataalamu wote wa SUA wafanye wanachoongea  kwa vitendo ili nwanafunzi aone uhalisia wake akijua hiyo ndio ajira yake na  vile vile wataalamu hao  kuwasukuma wanafunzi  katika kutenda zaidi uhalisia wa kupata matokeo.


"Muda wa kulalamika  umekwisha hatuna sababu tena kwa  sasa tuna rasilimali zote, mali na watu wamesoma wana ujuzi mkubwa ni wakati wa kutenda siyo kulalamika wala kutafuta ubaya uko wapi na wapi ,ni wakati wetu  kutenda na  inawezekana kila mtu akitimiza wajibu wake" amesema Prof.
  Muhairwa. 

Warsha hiyo imeandaliwa na Mradi wa TAGDev 2.0 AGRIFOSE–RIH ni sehemu ya Programu ya RUFORUM  kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo cha Nelson Mandela (Arusha), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), na Jukwaa la Vyuo Vikuu Afrika (RUFORUM) kwa ufadhili wa Mastercard Foundation ni mradi wa miaka 5.


Post a Comment

0 Comments