SUAMEDIA

Wanawake wametakiwa kusimamia malezi ya watoto ili kuzalisha vijana wenye maadili

 

Na: Siwema Malibiche

Wanawake wametakiwa kuwa na uangalifu mkubwa katika malezi ya watoto ili kubaini kwa haraka matukio ya ukatili yanayoweza kujitokeza katika familia ili kutengeneza vijana wenye weledi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Menejimenti Rasilimali Watu na Utawala Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Bw. Peter Mwakiluma kwenye hafla fupi iliyoandaliwa na Chuo hicho kupitia Kamati ya Maandalizi ya Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika Kimkoa katika halmashauri ya Mji Ifakara mkoani Morogoro.

Bw. Mwakiluma amesema wanawake wana wajibu mkubwa wa kulinda watoto kwa kushirikiana na vitengo mbalimbali vya haki zitakavyosaidia kuwajenga watoto na kuzalisha vijana watakaoleta maendeleo.

Aidha amewataka wafanyakazi wote wa SUA kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu ili kuendelea kukitangaza Chuo kwa utendaji bora wa kazi unaozingatia ufanisi na weledi na kwamba Menejimenti  ya Chuo itaendelea kuwawezesha wanawake wa SUA ili kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa sababu inatambua mchango wa wanawake katika Taasisi hiyo.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Morogoro Bi. Sidina Mathias ameupongeza uongozi wa SUA kwa kuanzisha Dawati la Jinsia  ambapo amewataka viongozi wa dawati hilo kushirikiana na Manispaa ili kuboresha huduma zinazotolewa  huku akitoa wito kwa wazazi na walezi kutojisahau katika malezi ya watoto.



Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake SUA ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani SUA Bi. Enesa Mlay ameishukuru Menejimenti ya SUA kwa kuwawezesha Wanawake wa Chuo hicho kuweza kushirikiana na wanawake wengine wa mkoa wa Morogoro huku akiwataka wazazi kutowaacha na kuwasahau  watoto wa kiume katika malezi yao.

Mratibu wa Masuala ya Jinsia kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Dkt. Charles Lyimo amesema SUA ni miongoni mwa Taasisi iliyokuwa na mazingira bora katika kusimamia watu wenye mahitaji maalum wakiwemo wanawake na amewataka kutumia ipasavyo dawati  la jinsia lililopo SUA ili kupata elimu na ushauri utakaosaidia kuijenga jamii.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa RAAWU Tawi la SUA Bw. Faraja Kamendu amewapongeza wanawake wote na wasichana walioshiriki katika Maadhimisho hayo huku akiwaasa kujiunga  na vyama vya wafanyakazi mahala pa kazi ili waweze kufaidika na maslahi yanayotokana na utetezi wa  kuwepo kwa sauti ya Pamoja.


Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mkoa wa Morogoro kimefanyika Machi 8 ,2025 katika Viwanja vya CCM Tangani  Halmashauri ya Mji Ifakara yakiwa
yamebeba kauli mbiu isemayo “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji”.











Picha zote na Nicholaus Roman

Zaidi bofya link hapo chini

https://drive.google.com/drive/folders/10PreFZrcI9NCWnosRiN_yXanwPUgk8dZ?usp=sharing





Post a Comment

0 Comments