Na:
Mwandishi wetu
Katika kukabiliana na changamoto za wafugaji na wakulima nchini, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wanaosomea masuala ya nyanda za malisho na ugani kilimo katika Idara ya Sayansi ya Wanyama, Viumbe Maji na Nyanda za Malisho wametakiwa kuzingatia mafunzo yanatolewa kuhusu nyasi za malisho zinazozalishwa hapa chuoni.
Meneja Shamba la Mafunzo SUA, Bw. Faridi Chamkwata amesema hayo wakati akiendelea kusimamia mafunzo kwa vitendo kwenye shamba la mafunzo kwa wanafunzi wakiwa wanavuna mbegu za nyasi aina ya rhodes, akisema elimu ambayo wanaitoa chuoni wakienda kuihamishia kwa wafugaji na wakulima katika jamii inaweza kupunguza migogoro ambayo imekuwa ikisikika kila mara.
Bw. Chamkwata amesema imekuwa kawaida kwa
wakulima kutofautiana na wafugaji lakini kama wafugaji wataelewa kuwa wanaweza
kuzalisha nyasi kama hizi (rhodes) kwa gharama ndogo na kupewa huduma ya ugani
karibu utakuwa mwisho wa migogoro.
"Sisi tunawafundisha kwa nadharia na vitendo, ili elimu hii wakitoka hapa watusaidie kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kuwaelimisha namna ya kujipatia nyasi nyingi katika eneo dogo, tena kwa gharama nafuu", alisema Bw. Chamkwata.
Nao baadhi ya wanafunzi ambao wanashiriki kuvuna
mbegu hizo wameelezea mafunzo hayo kuwa yanawapa uhalisia wa kujua vitu ambavyo
watakutana navyo baada ya kuhitimu masomo yao.
Samsoni Chalukula ambaye amejikita katika nyanda
za malisho na Devolta Danison Nicholaus ambaye anajihusisha na ugani kilimo
wamekiri kuwa mafunzo hayo ni muhimu katika maisha yao.
SUA imeendelea kutoa nafasi kwa wanafunzi
kushiriki katika mafunzo kwa vitendo ili kuwaongezea umahiri wanafunzi na
kuwapa uhalisia wa kile wanachojifunza darasani na nje ya darasa.
0 Comments