Na: Siwema Malibiche
Mkuu wa Wilaya ya
Kilombero Mhe. Wakili Dunstan Kyobya amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele kukemea
matendo ya ukatili ambayo yamekuwa yakitokea katika jamii kwa kutoa taarifa
katika vyombo husika ili kutengeneza jamii iliyo bora kwa maendeleo ya Taifa.
Akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima, Wakili Kyobya amevitaka vyombo vinavyoshughulikia masuala ya haki na sheria kushirikiana katika kutafuta haki huku akiwataka Wakurugenzi wa halmashauri zote kusimamia haki ipasavyo.
Katika maadhimisho hayo ambapo pia wanawake na wasichana kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameshiriki, Mkuu waWilaya amewakata wanawake na wasichana kote nchini kuchangamkia fursa za kiuchumi huku wakitumia nishati safi na salama ili kutunza mazingira kwa vizazi vijavyo kwa kuhakikisha kila mtu katika eneo lake anapikia nishati safi na salama ili kuepukana na uharibifu wa mazingira ambao unatokana na kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Wazazi Mkoa wa Morogoro Dkt. Kellen Rose Rwakatare amewasihi
Wanawake kuangalia maadili hasa katika makuzi ya watoto ili kukuza Taifa lililo
bora kimaadili.
“Siku hizi watoto wamekuwa wakiangalia TV na kuiga vitu
visivyofaa, wazazi tuwe macho katika hili, tusimamie maadili na nidhamu katika
makuzi ya watoto na Vijana wetu ili tukuze Taifa lenye Vijana wenye maadili na
nidhamu”, amesema Dkt. Kellen.
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mkoa wa Morogoro kimefanyika katika Viwanja vya CCM Tangani Halmashauri ya Mji Ifakara ambapo baada ya maadhimisho hayo Wanawake na Wasichana wa SUA kwa kushirikiana na Menejimenti ya Chuo hicho pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo wanaume walifanya tafrija fupi ikiwa ni sehemu ya kusherehekea siku hiyo.
0 Comments