SUAMEDIA

Utafiti SUA wabaini mabadiliko chanya katika tabia za ulaji wa vyakula mijini na vijijini

 Na: Ayoub Mwigune

 Utafiti uliofanywa kupitia Mradi wa Chakula, Kilimo na Lishe (FoodLAND) unaoratibiwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) umebaini mabadiliko makubwa katika tabia za walaji nchini hasa vijijini na mijini.


Akizungumza na wakazi wa Kata ya Dakawa Wilaya ya Mvomero wakati wa kufunga Mradi wa FoodLAND na kuanzishwa kwa Jukwaa la Wakulima, Dkt. Suleiman Rashid, Mhadhiri kutoka SUA amesema kuwa ingawa mabadiliko hayo ni chanya, bado kuna changamoto ya upungufu wa vyakula vyenye protini, hasa katika maeneo ya vijijini. 

 Utafiti huo ulifanyika katika maeneo ya wilaya ya Mvomero na Dar es Salaam na umeonesha kuwa tofauti ya ulaji wa vyakula kati ya maeneo hayo imekuwa ndogo zaidi kutokana na maendeleo katika uzalishaji na usafirishaji wa vyakula.

 


Dkt. Suleiman amesema vyakula ambavyo hapo awali vilionekana kuwa ni vya mijini pekee, kama vile chipsi na baadhi ya vyakula vya kukaanga, sasa vimekuwa vikipatikana vijijini kutokana na ongezeko la uzalishaji na maboresho katika usafirishaji.

 Aidha Dkt. Suleiman amesema hatua hiyo imeleta mabadiliko makubwa katika tabia za walaji kutokana na vyakula hivyo kupatikana maeneo yote jambo linaloonyesha maendeleo katika sekta ya kilimo na usafirishaji wa vyakula na kusema ni muhimu kuhamasisha jamii kuhusu lishe bora, hasa kwa kutumia vyakula vya asili ambavyo vilikuwa sehemu muhimu ya lishe kwa miaka mingi.

 "Vyakula vya asili vina virutubisho muhimu vinavyosaidia afya bora zaidi kuliko vyakula vya kisasa ambavyo mara nyingi vinaandaliwa kwa njia zisizo na tija kwa mwili" , amesema Dkt. Suleiman.

 


Kwa upande wao Fedrick Godfrey Swai, Mwasilima Guma Simba, na Pendo Ndemo, wakazi wa Mvomero, wamesema Mradi wa FoodLAND umewapa elimu ya kuongeza thamani katika kilimo na pia kukuza jukwaa walilolianzisha la kilimo.

 


Prof. Suzan Nchimbi Msolla, Mkuu wa Mradi wa FoodLAND, amesema kuwa Mradi huo umekuwa na mafanikio makubwa kama kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kilimo na ufugaji wa kisasa ili kuboresha lishe na kusisitiza kuwa ingawa mradi umefikia mwisho, SUA itaendelea kushirikiana na watafiti wengine wa lishe nchini ili kuhakikisha elimu hiyo inaendelea kusambazwa kwa jamii.








Post a Comment

0 Comments