SUAMEDIA

Mradi wa AGRISPARK kuzalisha vitabu vinavyojibu changamoto za wakulima nchini

 Na: Calvin Gwabara – Morogoro.

Watafiti wa mradi wa AGRISPARK kutoka Chuo Kikuu caha Sokoine cha Kilimo SUA wameanza utekelezaji wa mpango wa uandaaji wa vitabu vidogo vyenye lengo la kutoa majibu ya changamoto mbalimbali za wakulima nchini kwa kuwapatia mafunzo wanafunzi watafiti watakaoshiriki kwenye kuandaa vitabu hivyo.

Mtafiti Mradi wa Mbinu Shirikishi za Wanafunzi na Wakulima katika Uvumbuzi na Uhaulishaji wa Maarifa na Teknolojia za Kilimo (AGRISPARK) Dkt.Philbert Nyinondi akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo

Akifungua mafunzo hayo Mtafiti Mradi wa Mbinu Shirikishi za Wanafunzi na Wakulima katika Uvumbuzi na Uhaulishaji wa Maarifa na Teknolojia za Kilimo (AGRISPARK) Dkt.Philbert Nyinondi amewataka wataalamu hao kuzingatia mafunzo hayo ya awali ambayo yanalengo la kuwajengea msingi wa kazi hiyo ambayo wanatarajia kuanza kuifanya.

“Kwanza niwapongeze kwa kupata nafasi ya kushiriki kwenye kufanya kazi hii muhimu kati ya wanafunzi wengi wa Chuo chetu, Mtambue kuwa kazi hii mnayoifanya ni kwa maslahi ya wakulima na wafugaji wetu maana vitabu mtakavyoandaa tunatarajia vitasaidia kujibu changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wakulima na wafugaji na vitasambazwa kwa njia mbalimbali kuwafikia ikiwemo kupitia mfumo wa MKULIMA LIBRARY uliopo kwenye Maktaba ya Taifa ya Kilimo” alifafanua Dkt. Nyinondi.

Mkuu huyo wa mradi wa AGRISPARK amesema baada ya mafunzo hayo watapata nafasi ya kwenda kwenye maeneo mbalimbali ya mradi ikiwemo Wilaya ya Mvomero, Manispaa ya Morogoro na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini kwaajili ya kukutana na wakulima na kuzungumza nao katika mazingira halisi ili kupata taarifa mbalimbali kuhusu mada za vitabu wanavyoviandaa.

Aidha Dkt. Nyinondi amewataka kuzingatia mambo mbalimbali wakutanapo na wakulima vijijini ikiwemo swala la matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili kwa kutochanganya na lugha ya kiingereza kwenye mazungumzo yao,Mavazi, Maadili ya jamii husika pamoja na kutowaona wakulima kama hawajui bali watambue kuwa wana uzoefu wa miaka mingi na wanajua vitu vingi ambavyo wao hawajui.

Nae kwa upande wake mtafiti mkuu mwenza wa Mradi huo wa (AGRISPARK) Dkt. Nicholaus Mwalukasa amesema wakati wa mafunzo hayo watapitishwa kwenye mada mbalimbali ili kuwajengea uwezo katika kutekeleza kwa ufanisi zoezi hilo ikiwemo mnyororo wa thamani wa mazao mbalimbali, Kilimo bora cha mazao, masuala ya masoko, Mbegu bora za kilimo pamoja na namna ya kuandaa vitabu hvyo.

“Mafunzo haya tumeona ni muhimu sana kwenu kufanyika kabla ya kuanza kazi kubwa iliyo mbele yenu, na tunaamini baada ya mafunzo haya na kuelewa upana wa kazi hii na matarajio ya mradi mtaweza kufanya kazi nzuri ambayo itakuwa na mchango mkubwa kwa wakulima wetu na taifa kwa ujumla wake” Alisisitiza Dkt. Mwalukasa.

Dkt. Mwalukasa amesema kazi inayofanyika ni sehemu ya utekelezaji wa wa malengo ya mradi huu ya kutumia Mbinu Shirikishi za Wanafunzi na Wakulima katika Uvumbuzi na Uhaulishaji wa Maarifa na Teknolojia za Kilimo  kwa kutengeneza vijitabu vizuri ambavyo vitasaidia kufikia lengo hilo.

Mtafiti mkuu mwenza wa Mradi huo wa (AGRISPARK) Dkt. Nicholaus Mwalukasa akitoa neno kwa washiriki hao wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake Hawa Twaibu amewahakikishia viongozi wa mradi huo na SUA kuwa watafanya kazi kwa bidii katika kuhakikisha wanatimiza malengo ya mradi kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa katika kipindi chote watakachukuwa kwenye zoezi hilo.

“Tunashukuru Mradi wa AGRISPARK na Chuo kwa kutupa nafasi ya kufanya kazi hii muhimu kwa wakulima wa Tanzania, na tunaamini kupitia kazi hii itatupatia uzoefu mkubwa kwenye kuteleza mazoezi ya aina hii siku zijazo na kutusaidia kuweza kujua namana ya kufungasha elimu na kuifikisha kwa wakulima na wahitaji wengine” Alisema Hawa.

Mradi wa AGRISPARK Ulizinduliwa mwishoni mwa kwama 2024 na Rasi wa Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi (CoNAs) Dkt. Geofrey Karugila kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda na unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chuo Kikuu cha Sokine cha Kilimo SUA kama maono makubwa ya Chuo katika kuinua watafiti wake hasa wachanga kwa kutenga fedha za ndani ili wafanye tafiti za kusaidia kutatua changamoto za jamii na taifa.

Matukio katika picha Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia maelekezo na nasaha za ufunguzi.









Post a Comment

0 Comments