Na: Ayoub Mwigune
Akizungumza wakati wa hitimisho la Mradi wa Chakula, Kilimo na Lishe (FoodLAND), Mhadhiri Mwandamizi na Mtaalamu wa Ufugaji na Uvuvi wa Samaki Dkt. Renalda Mnubi kutoka SUA amesema lengo kuu la mradi huo lilikuwa ni kuwawezesha wafugaji kwa kuwafundisha mbinu bora za ufugaji wa samaki pamoja na kuwapatia elimu ya vitendo, ili waweze kuzitumia katika mazingira yao ya kila siku.
Dkt. Renalda ameongeza kuwa uzalishaji wa chakula cha samaki kwa njia binafsi uliwasaidia wafugaji kuondoa changamoto kubwa iliyowakumba katika ununuzi wa chakula cha samaki.
"Uwezo wa kuzalisha chakula cha samaki wenyewe uliwaondolea utegemezi wa wafugaji kwa wauzaji wa chakula cha samaki, jambo ambalo liliongeza faida yao na kuboresha uzalishaji" amesema Dkt. Renalda.
Kwa upande wao, Mariam Bakari na Festo Liguduliaka, wakazi wa Kijiji cha Mshikamano, Kata ya Mang'ula B, Halmashauri ya mji wa Ifakara mkoani Morogoro, ambao ni wanufaika na mradi huo, wameshukuru SUA kwa kuwapatia elimu hiyo muhimu ambayo imewawezesha kupata maarifa yaliyoboresha ufugaji wa samaki katika familia zao na kuinua hali yao ya kiuchumi.
Naye Mratibu wa Mradi huo kwa upande wa Tanzania, Prof. Suzan Nchimbi Msolla amesema kuwa lengo kuu la FoodLAND lilikuwa kuboresha lishe ya Watanzania kwa kuwapatia elimu kuhusu matumizi ya vyakula mbalimbali ili kujenga afya bora.
0 Comments