SUAMEDIA

Waandaaji wa vitabu vya elimu kwa Wakulima wapewa misingi ya uandaaji wake ili vilete tija.

 Na: Calvin Gwabara – Morogoro.

Watafiti wanafunzi kupitia mradi wa AGRISPARK wametakiwa kuhakikisha wanazingatia kanuni na sheria za uandaaji wa Vitabu vya elimu kwa wakulima ili viweze kusomeka vuzuri na kueleweka na kila mkulima ili elimu iliyomo iweze kuwasaidia.

Msimamizi wa kitengo cha rejea na huduma za Makataba kwa jamii kutoka Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya Kilimo SUA Bwana Jabir Jabir akiwasilisha mada yake.

Wito huo umetolewa na Msimamizi wa kitengo cha rejea na huduma za Makataba kwa jamii kutoka Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya Kilimo SUA Bwana Jabir Jabir wakati akifundisha akifundisha timu ya Wataalamu Wanafunzi wa mradi wa AGRISPARK namna ya kufanya usanifu na uhariri wa taarifa kwaajili ya kuandaa vitabu vya Elimu Kwa wakulima.

“Wakati mtakapoanza  kuandaa vitabu vya elimu kwa wakulima kuhusu mbinu bora za kilimo na ufugaji, ni muhimu kutumia lugha rahisi na inayoeleweka kwa wakulima wengi maana lugha inapaswa kuwa fasaha lakini isiyo na maneno magumu ya kitaalamu yasiyoweza kufahamika kirahisi na wakulima wa kawaida lakini pia matumizi ya mifano halisi yanayohusiana na mazingira ya wakulima husika yatawasaidia kuelewa na kuhusisha maelezo na maisha yao ya kila siku, hivyo kuongeza uelewa na utekelezaji wa maarifa wanayopata” alisema Jabir.

Msimamizi huyo wa kitengo cha rejea na huduma za Makataba kwa jamii kutoka Maktaba ya Taifa ya Sokoine ya Kilimo (SNAL - SUA) amesema muundo wa kitabu unapaswa kuwa wa kuvutia na rahisi kusomeka, ukiwa na maandishi yaliyopangiliwa vizuri, vipengele vilivyogawanywa kwa utaratibu, na matumizi ya vielelezo kama picha, michoro na jedwali.

Jabir amesema vielelezo hivyo vinasaidia kuelezea hatua kwa hatua mbinu bora za kilimo na ufugaji, hasa kwa wakulima wasiojua kusoma vizuri lakini wanaweza kuelewa kwa kuona na ni muhimu kuhakikisha kuwa kila sura inajengwa kwa mtiririko mzuri wa maarifa, kuanzia dhana za msingi hadi mbinu za hali ya juu, ili msomaji aweze kujifunza kwa utaratibu mzuri.

“Maudhui ya vitabu vinavyohusu kilimo na ufugaji yanapaswa kuwa sahihi na kuzingatia hali halisi ya mazingira ya kilimo ya wakulima husika, hii inamaanisha kuwa vitabu vinapaswa kuzingatia aina ya udongo, hali ya hewa, mbegu bora, mifugo inayofaa, na mbinu za kisasa zinazotumika katika maeneo husika kwa kuzingatia tafiti za hivi karibuni na ushauri wa wataalamu wa kilimo na ufugaji zinapaswa kuzingatiwa ili kutoa taarifa zilizo sahihi na zinazoweza kutekelezeka kwa urahisi na wakulima.

Aidha Jabir amewema vitabu hivi vinapaswa kuwa na sehemu za maswali na majibu, hadithi fupi za mafanikio ya wakulima waliotumia mbinu husika, na hata maelezo ya wapi wakulima wanaweza kupata msaada zaidi.

Kuwashirikisha wakulima katika uandishi wa vitabu hivi pia ni muhimu, kwani watatoa ushuhuda wa changamoto wanazokutana nazo na mbinu zilizowasaidia na kwa kufanya hivyo, vitabu vitakuwa na uhalisia zaidi na vitawafanya wakulima kuviona kama nyenzo halisi za kuwaongoza katika kuboresha shughuli zao za kilimo na ufugaji.


MATUKIO KATIKA PICHA WASHIRIKI WIKIFUATILIA MAFUNZO.














Post a Comment

0 Comments