SUAMEDIA

Zoezi la kuboresha sera za kilimo linaendelea - Msemaji Mkuu wa Serikali

 Na: Gerald Lwomile

Serikali imesema pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la Kahawa kutoka tani 55 elfu hadi kufikia tani 85 elfu katika kipindi cha miaka 3 inafanya maboresho makubwa ya sera zake za kilimo kwani zimekuwa kikwazo katika kuleta maendeleo ya kilimo nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu ka Serikali Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari

Hayo yamesemwa tarehe 16 februari, 2025 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa kuhusu masuala mbalimbali yaliyotekelezwa na serikali wakati wa mkutano   na waandishi wa habari katika Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere Rufuji mkoani Pwani.

 Akizungumzia uzalishaji wa zao la Kahawa nchini Msemaji Mkuu wa Serikali amekiri kuwa sera mbalimbali za Serikali kwa wakati fulani zimekuwa si rafiki na kupelekea changamoto katika kilimo na soko la Kahawa nchini.

Msigwa amesema hivi sasa takwimu  zinaonesha kuwa kuna nchi 50 zinazozalisha kahawa duniani ambapo kati ya hizo bara la Afrika ni  25 na kuwa nchini Tanzania uzalishaji wa kahawa katika kipindi cha miaka 3 umeongezeka kutoka tani 55 elfu hadi tani 85 elfu.

Amesema tarehe 21 na 22 Februari, 2025 Tanzania itakua mwenyeji wa mkutano wa tatu wa Afrika wa Kahawa G25, utakaofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Tarehe 1 Juni, 2022 Mkuu wa Mradi wa utafiti wa 'TRADE HUB' Prof. Ruben Kadigi akitoa matiokeo ya awali ya utafiti juu ya kutambua faida za kiuchumi, kijamii na kimazingira zinazotokana na biashara ya Kahawa nchini alitaja changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na sera pamoja na bei ya Kahawa kutokuwa rafiki katika uwekezaji wa zao hilo.

Akizungumzia suala la Umeme msemaji wa Serikali amesema watanzania wawe na subira juu ya gharama za umeme kwani  kuwa juu kwani inaangalia namna bora zaidi ya kuhakikisha umeme unakuwa  na gharama nafuu tofauti na sasa.

Amesema nchi imefanya uwekezaji mkubwa katika uzalishaji wa umeme kwani mbali na kuwa na Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere Rufiji mkoani Pwani ina miradi kadhaa mingine mingi ikiwa ni pamoja na mradi wa Rusumo utakaozalisha Megawati 80, Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Gesi Asilia wa Kinyerezi ‘I Extension’ utakaozalisha Megawati 185.

Ametaja Miradi mingine ni Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Malagarasi Megawati 49.5 Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Kakono Megawati 87 na Mradi wa umeme wa jua ulianzishwa katika Wilaya ya Kishapu Mkoani wa Shinyanga wenye uwezo wa kuzalisha jumla ya Megawati 150.

Kusikiliza zaidi bofya 👇

https://www.youtube.com/watch?v=mgvm78YIkyU

Post a Comment

0 Comments