Na: Gerald Lwomile
Serikali
imesema ujenzi wa Mradi wa Julius Nyerere Hydropower Project (JNHPP) wenye
uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 ulioanza mwezi Juni 2019 umefikia asilimia 99.8 na mpaka sasa, jumla ya
mashine 8 kati ya 9 zimeshawashwa na kufanya jumla ya Megawati 1,880 kuongezeka
kwenye Gridi ya Taifa ya Umeme.
![]() |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari |
Hayo yamesemwa tarehe 16 Februari, 2025 na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson
Msigwa katika mkutano wake na vyombo vya habari uliofanyika katika Bwawa la kufua
umeme la Julius Nyerere, Rufiji mkoani Pwani.
Msigwa amesema mradi huu ambao uliachwa ukiwa na
asilimia 33 tu na Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli umekuwa na maendeleo
mazuri kwani Mhe. Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan
amehakikisha miradi yote iliyoachwa na mtangulizi wake inaendelea katika
viwango vya hali ya juu.
Msemaji wa Serikali amesema tuta kuu ambalo hutumika
kuhifadhi maji ya kuzungusha mashine kwa ajili ya kufua umeme ujenzi wake
umekamilika kwa asilimia 100 na lina Urefu wa mita
1,036; kina cha mita 131 na lipo kwenye eneo la kilomita za mraba 914 na lina
uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo bilioni 32.8.
![]() |
Bwawa la JNHPP |
Msigwa amesema mahandaki matatu ya
kusafirisha maji kuelekea kwenye mitambo nayo yamekamilika kwa asilimia 100 na jengo
la mitambo likiwa na mitambo tisa ya kuzalisha umeme ambapo kila mmoja ina uwezo
wa kuzalisha megawati 235 nalo limekamilika kwa asilimia 99.
Msigwa amesema sehemu nyingine ambayo imetiliwa mkazo ni utekelezaji wa Mradi wa kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi Chalinze wa kilo voti 400, yenye urefu wa km 160 ambao sasa umefikia asilimia 99.5 ikilinganishwa na asilimia 44 mwaka 2021/22.
Aidha, ujenzi wa kituo
cha kupoza Umeme cha Chalinze ambacho ni sehemu ya mradi huo umefikia asilimia 92
ikilinganishwa na asilimia 35.9 mwaka 2021/22. Ukamilishwaji wa miundombinu hii
imewezesha umeme kusafirishwa kutoka kituo cha kuzalisha umeme cha JNHPP hadi
Chalinze na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.
Msigwa
amesema thamani ya ujenzi
wa Mradi wa JNHPP ni Shilingi tririon 6.558 ambapo hadi kufikia mwezi Februari
2025, mkandarasi alimelipwa kiasi cha Shilingi Bilioni 6.3 ambacho ni sawa na
asilimia 95.9.
Amesema kukamilika kwa mradi huo ni mingine inayoendelea nchini utasababisha nchi kuzalisha umeme mwingi wa mege wati 4000 wakati mahitaji ya ndani ni mege wati 1900 hivyo kuwa na umeme unaoweza kuuzwa nje ya nchi ikiwa ni pamoja na Zambia na Kenya.
0 Comments