Na; Georgr Alexander
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) kimepongezwa kwa kuendelea kuwa Chuo Kikuu Kiongozi katika sekta ya kilimo
nchini kupitia wataalam wake na tafiti zake pamoja na wadau mbalimbali wa ndani
na nje ya nchi.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Mahela wakati wa uzinduzi wa Kigoda cha Ushirikiano wa kubadilishana Maarifa kati ya Japani na SUA kwa kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kupitia mradi ujulikanao kama JICA CHAIR uliofanyika SUA.
Dkt. Mahela amesema kwa miaka
yote tangu kuanzishwa kwake SUA imekuwa Chuo Kiongozi hapa Tanzania kwa kufanya
tafiti zenye kutatua changamoto za wananchi hususan wakulima ambapo
kwa sasa kupitia JICA watawawezesha wanafunzi wengi kujifunza kilimo cha
umwagiliaji.
Akizungumzia kuhusu Kigoda cha Ushirikiano Dkt. Mahela amesema kupitia Kigoda hicho Serikali ya Japan na Tanzania kupitia Chuo cha SUA kitawawezesha kukaa na wataalam na Maprofesa mbalimbali na wataweza kufanya tafiti za kuweza kuwa na kilimo cha kisasa hususani cha umwagiliaji.
“Tutawatumia Japan katika
kuendeleza kilimo chetu hususani kilimo cha umwagiliaji na ukiangalia Japan ni
nchi ndogo lakini yenye mafanikio makubwa katika kilimo, ambapo wanalima sehemu
ndogo lakini uzalishaji unakuwa mkubwa sana” amesema Dkt. Mahela.
Aidha amesema Serikali ya awamu
ya 6 imewekeza zaidi kwenye kilimo na inataka kuwa na kilimo chenye tija hapa
nchini na hivyo kwa Tanzania ni fursa kubwa kupitia JICA, maana itatoa elimu
kwa wanafunzi ambao wao wanakwenda moja kwa moja kuhudumia jamii kote nchini.
Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Balozi Mikami Yoichi ikiwa ni mara yake ya kwanza kufika SAUA tangu kuteuliwa kwake kuwa Balozi amesema ushirikano huo utaleta maendeleo katika sekta ya kilimo na hivyo Japan kupitia JICA itaendelea kushirikiana na SUA katika kilimo.
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu
wa Chuo Taaluma, utafiti na ushauri wa Kitaalam Prof.
Maulid Mwatawala kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema
Japan kama inavyojulikana ni nchi ambayo imepiga hatua kubwa katika miundombinu
na teknolojia za umwagiliaji hivyo SUA itanufaika kupitia mabadilishano hayo
katika umwagiliaji.
Aidha Prof. Mwatawala amebainisha kuwa SUA ni Chuo ambacho kimekathimishwa kwa kutoa elimu ya uhandisi kilimo nchini hivyo kinatakiwa kutoa elimu kulingana na mahitaji ya jamii kwenye kilimo ili kukabiIiana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame, hivyo ushirikiano huu katika sekta ya umwagiliaji utawasaidia wanafunzi kulingana na sera na agenda mbalimbali za Serikali katika sekta ya kilimo.
“Hivi karibuni Rais Samia akiwa
katika mkoa wa Ruvuma alisema lengo la nchi ni kuongeza kilimo cha umwagiliaji
kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 kwa hiyo ni lengo kubwa sana, pia katika
agenda ya 2030 ya Wizara ya Kilimo ni kuongeza kilimo cha umwagiliaji kufikia
hekta milioni nane” amesema Prof. Mwatawala.
Kwa upande wao wanafunzi
walioshiriki Kigoda hicho wamepongeza ushirikiano huo ulioanzishwa na SUA kwa
lengo la kubadilishana maarifa ya kiteknolojia kwa wanafunzi na kuwa utawasaidia
katika soko la ajira hapo baadaye.
Katika mabadilishano hayo
wanafunzi wanaosoma SUA wataweza kufundishwa teknolojia mbalimbali katika
kilimo cha umwagiliaji kutoka kwa wataalam nchini Japan wakishirikiana na
wataalam kutoka SUA.
0 Comments