SUAMEDIA

Wanataaluma SUA wametakiwa kujitokeza na kuonesha umahiri wa kazi zao

 

Na: Winfrida Nicolaus

Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wametakiwa kujitokeza ili kuuonesha umma na Taifa kwa ujumla maeneo yao ya umahiri na nini wamefanya na namna wanavyoweza kuisaidia jamii ya watanzania pamoja na Chuo kupitia maeneo hayo zikiwemo tafiti zao.


Amebainisha hayo Dkt. Kassim Mussa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma wa SUA (SUASA) kwenye moja ya mfululizo wa Mihadhara ya Wanataaluma chuoni hapo wakati akizungumza na SUA Media ambapo amesema dhumuni la mfululizo wa mihadhara hiyo ni kutaka kufahamu wanataaluma waliotoka masomoni wamefanya nini na wana kitu gani cha kuwaambia kuhusu tafiti zao hasa kwenye maeneo yao ya ubobezi.

Amesema faida ya kufanya mfululizo wa mihadhara kwa wanataaluma ni kuwasaidia kuwafahamu watu na maeneo yao ya umahili na endapo wakiwa wanatafuta watu wa kusaidia kwenye kazi mbalimbali chuoni hapo basi ni lazima wakafahamu nani yuko wapi na amefanya nini.

Aidha Dkt. Kassim amesema mwanataaluma kokote duniani anafahamika kwa ufanisi na umahili hivyo hawawezi kufahamu ufanisi na umahili wa wanataaluma walionao kama hawatawaita na kufanya mfululizo wa uwasilishaji wa mihadhara ya wanataaluma hao.

“Kimsingi tunako elekea ni kuzuri sana na kama tulivyoazimia hivi sasa tumefanya ni tabia kwa wanataaluma hivyo tutakua tunaitana mara kwa mara na Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam imeahidi kushirikiana na SUASA ambayo nayo  imeahidi kutoa ushirikiano na kupitia hii Taasisi itakuwa imejitangaza sana ulimwenguni na kujulikana zaidi”, amesema Dkt. Kassim.

Kwa upande wake mmoja wa washiriki katika mhadhara huo Bi. Jenipher Tairo Mhadhiri Msaidizi kutoka Idara ya Mimea Vipando na Mazao ya Bustani SUA amesema Mihadhara hiyo ni mizuri sana kwa sababu inawapatia fursa ya wao kujua kile walichokifanya kwenye tafiti zao lakini pia matokeo ya tafiti hizo katika kuisaidia jamii na taifa kwa ujumla.

Amewahamasisha wanataaluma kuweza kuhudhuria mihadhara hiyo kwa sababu watapata fursa ya kujifunza zaidi kutoka kwa wengine lakini pia kujiongezea wigo wa kufahamiana zaidi na wanataaluma wenzao katika kile wanachokifanya kwa kuwa wanaweza kufanya vitu tofauti lakini lengo lao ni moja, kuisaidia jamii na Taifa kwa ujumla.

“ Tunaupongeza uongozi wa Chuo kwa kuja na wazo hili na tunaomba liwe endelevu kwa sababu lina faida sio tu kwa wakufunzi wa SUA lakini pia kwa jamii yetu maana itajua matokeo ya tafiti zetu ni yapi na kwa namna gani zinaweza kuwanufaisha”, amesema Bi. Jenipher.



Post a Comment

0 Comments