SUAMEDIA

Wafanyakazi wametakiwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kuwa na sauti ya pamoja

 

Na: Siwema Malibiche

Wafanyakazi nchini wametakiwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi ikiwemo RAAWU ili kusaidia kuwa na sauti ya pamoja mahala pa kazi itakatowezesha kuboresha namna ya utekelezaji wa majukumu yao kwa kufuata haki na wajibu.



Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa RAAWU Tawi la SUA Bw. Faraja Kamendu baada ya kumalizika kwa Semina ya wafanyakazi wa SUA na Wanachama wa RAAWU Tawi la SUA iliyofanyika Kampasi ya Edward Moringe mjini Morogoro ambapo amewasisitiza wafanyakazi kuona umuhimu wa kujiunga na vyama vya wafanyakazi kwa maslahi yao binafsi na kwa taifa.

Amesema  RAAWU imemua kufanya semina hiyo baada ya kufanya tafiti mbalimbali  na kugundua kuwa wafanyakazi wengi hawana elimu ya kustaafu na namna ya kuwekeza wanapokuwa kazini na kuamua kuja na mafunzo kwa wastaafu watarajiwa kwa kuwajengea uwezo utakaosaidia  kuyaelewa mazingira yao baada ya kustaafu kwa kuwekeza ili kuepuka changamoto


Kwa upande wake, Katibu wa RAAWU Mkoa wa Morogoro Bi. Agness Gwau amesema uongozi wa chama hicho umeamua  kutoa mafunzo hayo ili kuwajengea misingi bora ya kiuwekezaji kwa wafanyakazi na kuongeza kuwa kama uongozi  utaendelea kuyaleta mafunzo mara kwa mara ili kuwajenga kiutendaji wanachama wake

Naye  Mmoja wa washiriki katika Semina hiyo Bw. Haroun Kapingo  ambaye ni Mtumishi kutoka SUA amesema semina hiyo imekuwa ni ya manufaa zaidi  kupitia mafunzo waliyopewa kwani imewapatia uelewa wa haki na wajibu wao kama wafanyakazi  na namna nzuri ya kujiandaa katika uwekezaji kabla ya kustaafu.

Aidha ameupongeza uongozi wa RAAWU SUA  kwa kuyaleta mafunzo hayo ya siku mbili kwa wafanyakazi ambayo anaamini yataleta tija huku akiwasisitiza washiriki wote wa mafunzo hayo kutekeleza kwa vitendo yale yote waliyojifunza ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza wakiwa kazini na baada ya kustaafu.

Semina hiyo ya siku mbili kwa wanachama wa RAAWU na wafanyakazi wa SUA ambayo imeandaliwa na chama cha RAAWU Makao Makuu kwa kushirikiana na RAAWU Tawi la SUA imewawezesha washiriki kujifunza elimu ya vyama vya wafanyakazi, njia za kusaidia katika ukuaji wa taaluma kazini na maandalizi ya kustaafu.

Kauli mbiu ya chama hicho ni “Elimu kwanza, Nguvu ya hoja, Kwa maslahi bora ya Wafanyakazi.





Post a Comment

0 Comments