Na: Farida Mkongwe
Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kusimamia na
kutenda haki na usawa katika kuhabarisha jamii kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2025 ili wananchi wapate elimu itakayowasaidia kufanya uchaguzi sahihi wa viongozi
watakaowaongoza na kuliongoza Taifa kwa ujumla.
Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi na wawakilishi wa Wakurugenzi wa vyombo vya habari nchini. |
Kauli hiyo imetolewa Februari 13, 2025 na Waziri wa
Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi wakati akifungua Mkutano
wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji Nchini unaofanyika jijini Dodoma.
Prof. Kabudi amesema vyombo vya habari vya utangazaji
nchini kupitia vipindi mbalimbali vina nafasi kubwa ya kutoa elimu kwa jamii na
kuijengea uelewa utakaochangia katika upatikanaji wa viongozi bora watakaoleta
maendeleo nchini.
Aidha Prof. Kabudi ametoa wito kwa vyombo vya habari
nchini kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu utabiri wa hali ya hewa unaotolewa
na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili jamii ichukue tahadhari kuhusu
athari za mabadiliko ya tabianchi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) Dkt. Jabir Kuwe Bakari amesema mamlaka hiyo ina imani kupitia mshauri wa
kitaalam kutoka Uingereza anayefanya kazi na mamlaka hiyo wanatajia kuja na sera
nzuri za usimamizi wa vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na kupitiwa upya kwa
gharama mbalimbali ikiwemo gharama za leseni ambazo mara kadhaa zimelalamikiwa
kuwa ni kubwa.
Mkutano huo wa siku mbili wa Mwaka wa Vyombo vya
Utangazaji Nchini uliobeba Kauli Mbiu isemayo “Wajibu wa Vyombo vya Utangazaji
Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025" umeenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Redio
Duniani ambayo yamebeba Kauli Mbiu isemayo “Redio na Mabadiliko ya Tabianchi”.
0 Comments