Na: Siwema Malibiche
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimekipongeza Chama
cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Ufundi Stadi,
Habari na Utafiti (RAAWU) kwa kuendelea kuzungumzia na kusimamia maslahi ya
haki na wajibu kwa wafanyakazi wa SUA huku kikiwataka wafanyakazi kufuata taratibu, kanuni na sheria
za utumishi wa umma ili kufikia malengo ya Chuo kwa maendeleo ya taifa.
Pongezi hizo zimetolewa Februari 18, 2025 na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho anayeshughulikia Mipango, Utawala, na Fedha, Prof. Amandus Muhairwa wakati akifungua Semina ya Wanachama RAAWU Tawi la SUA na waajiriwa wapya iliyofanyika Kampasi ya Edward Moringe mjini Morogoro ambapo amesisitiza kuwa wafanyakazi wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kuchochea maendeleo nchini.
Prof. Muhairwa amesema Chama cha Wafanyakazi RAAWU kinafanya kazi kubwa ya kutetea maslahi bora ya wafanyakazi hivyo amewataka wafanyakazi nao kuzingatia maslahi ya mwajiri na matumizi sahihi ya muda ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa RAAWU Taifa Bi. Jane Mihanji
ameupongeza uongozi wa Chama cha Wafanyakazi RAAWU Tawi la SUA kwa kufanya kazi
zenye ubora na kuwa mfano wa kuigwa kwa matawi yote nchini huku akisema kuwa
anafurahi kuona viongozi wanatekeleza majukumu yao ipasavyo.
Pia amewataka wafanyakazi wote ambao wameshiriki katika semina hiyo kuambiana ukweli inapotokea mmoja wao anakiuka wajibu wake ili kuepuka kuunda makundi yatakayoharibu weledi na uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa RAAWU Tawi la SUA Bw.Faraja Kamendu amesema wao kama viongozi wataendelea kusimamia maslahi ya wafanyakazi yatakayoleta tija huku akiwataka wafanyakazi kuendelea kushirikiana na kushikamana na amewakaribisha wafanyakazi wote waliopo SUA kujiunga na chama hicho ili waweze kufaidika na maslahi yanayotokana na utetezi wa RAAWU.
Semina hiyo imeandaliwa na Chama cha Wafanyakazi RAAWU Makao
Makuu kwa kushirikiana na RAAWU Tawi la SUA ambapo kwa siku ya Jumanne Februari
18, 2025 imefanyika semina kwa wanachama wa Chama hicho na waajiriwa wapya wa
SUA na Februari 19, 2025 ilikuwa ni semina kwa wafanyakazi wote wa SUA.
0 Comments