Na: Ayoub Mwigune
Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) kimeendelea kuonesha mchango wake mkubwa katika sekta ya mifugo
kwa kuanzisha mradi wa utafiti wa NANO COMM, unaolenga kutengeneza tiba mbadala
ya homa ya kiwele kwa wanyama wanaotoa maziwa.
Kupitia utafiti huu, SUA inalenga kutatua changamoto sugu inayowakabili wafugaji wengi nchini, hususan katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Arusha, na Tanga.
Akizungumza na SUAMEDIA Prof.
Gaymary Bakari, Mhadhiri wa SUA na Mtafiti Kiongozi wa Mradi amesema utafiti
huu ni moja ya juhudi za Chuo hicho katika kutafuta suluhisho la changamoto za
wafugaji kupitia sayansi na tafiti.
"Tumebaini kuwa homa ya
kiwele imekuwa tatizo sugu kwa wafugaji wa wanyama wa maziwa na wengi wao
wanakosa tiba sahihi au wanatumia gharama kubwa kutibu mifugo yao",
amesema Prof. Bakari.
Prof. Gaymary amesema kuwa matarajio ya mradi huo ni kuleta suluhisho la moja kwa moja kwa wafugaji, kusaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa, kupunguza gharama za matibabu na kuimarisha uchumi wa wafugaji.
Ameongeza kuwa kwa miaka mingi, SUA imekuwa
kinara wa tafiti mbalimbali zinazolenga kuboresha afya ya mifugo na uzalishaji
wa mazao yake.
Aidha, Prof. Gaymary Bakari
ameomba jamii kutoa ushirikiano wa karibu kwa mradi huu ili kufanikisha malengo
yake huku akisisitiza kuwa ushirikiano wa jamii, hususan wafugaji na wadau wa
mifugo, utakuwa muhimu katika kuhakikisha kuwa tiba zinazopatikana zinakuwa
sahihi na zinafanikiwa kutatua changamoto za kiwelea katika sekta ya mifugo.
"Tutahitaji kutoa msaada kwa wafugaji na jamii kwa ujumla ili tuweze kupata suluhisho bora litakalosaidia sekta hii kubwa na muhimu", amesema Prof. Bakari.
Ezekia Mbalwa na Lisa Kisanga,
ni wanafunzi wa Shahada ya Uzamili SUA, ambao ni watafiti washiriki katika
mradi huu ambapo wameeleza kuwa mbali na kushiriki katika utafiti, mradi huo
umewasomesha katika Shahada zao za Uzamili, jambo lililowapa fursa ya kupata
ujuzi wa kina kuhusu tiba za mifugo na tafiti za kimataifa.
"Tunaamini kuwa kupitia
utafiti huu, SUA itaendelea kuwa chombo muhimu cha mabadiliko chanya katika
sekta ya mifugo nchini," amesema Mbalwa.
0 Comments