SUAMEDIA

Wanafunzi SUA watakiwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Chuo

 Na: Siwema Malibiche

Wanafunzi wapya waliochaguliwa kujiunga na masomo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa mwaka wa masomo 2024/2025 wametakiwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa huku wakisoma kwa bidii zitakazowawezesha kutimiza malengo yao waliyojiwekea.

                        

Hayo yamebainishwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda wakati wa kufunga wiki ya mapokezi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza iliyofanyika ndani ya Kampasi ya Solomon Mahlangu mkoani Morogoro ambapo amewataka wanafunzi hao kuishi katika malengo waliyojiwekea huku akisema Menejimenti ya SUA imeandaa miondombinu bora ya kujifunzia na itaendelea kuboreshwa.

Aidha amesema uongozi wa Chuo hautafumbia macho vitendo vyovyote vinavyoashiria ukatili wa kijinsia chuoni hapo na  ameongeza kuwa sheria kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya ukatili wa aina yoyote  huku akiwahasa wanafunzi wote kuishi katika maadili yanayostahili kwa jamii.            

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Utawala na Fedha SUA Prof. Amandus Muhairwa amesema SUA  itaendelea kujenga na  kuboresha miundombinu kupitia mradi wa  HEET katika kampasi zake zote kwa kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu ili kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Aidha amewataka wanafunzi wote ambao ni wanufaika na mkopo  wasisite kufika katika ofisi za mikopo chuoni na jumuiya ya wanafunzi chuoni  hapo wanapopata changamoto yoyote ya kifedha  ili kupata ufumbuzi wa haraka na  wenye kuepusha madhara ambayo yanaweza kujitokeza kutokana na wanafunzi kutotoa taarifa.

Kwa upande wake Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia SUA Prof. Samwel Kabote ambaye amemwakilisha  Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala amesema wanafunzi waliochagua kujiunga na masomo SUA wamefanya chaguo sahihi kutokana na Chuo hicho kuwa na mazingira mazuri ya kusoma ikwemo maktaba, itakayowawezesha kusoma machapisho mbalimbali, huduma za afya na ulinzi madhubuti na ni vyema kutumia ipasavyo.

Nao  wanafunzi wa mwaka wa kwanza Bw. Daudi Adrea na Bi. Laura Koka ambao ni wanafunzi waliojiunga na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo  wameupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa maandalizi mazuri ya kuwapokea huku wakiwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuepukana na makundi mabaya yatakayowafanya kutotimiza malengo yao.

                              

 

 

Post a Comment

0 Comments