Na: Calvin Gwabara – Morogoro.
Wakulima wa zao la Nyanya mkoani
Morogoro wamewataka wazalishaji na wasambazaji wa mbegu bora za nyanya nchini
kuleta mbegu mpya au kuziboresha mbegu bora zilizopo sokoni ambazo
zinashambuliwa sana na ugonjwa wa mnyauko na kuathiri tija kwa wakulima wa zao
hilo.
Wadau wa kilimo Wilaya ya Mvomero na Manispaa ya Morogoro wakiangalia shamba darasa la mradi wa SUA - Fair Planet. |
Akitoa uzoefu wake Mkulima
maarufu wa nyanya mkoani Morogoro bw. Khalid Gumbo amesema wao wanalima nyanya
kutokana na uhitaji wa soko na soko linataka nyanya ambazo zina ganda gumu
linalowezesha nyanya kukaa muda mrefu sokoni bila kuharibika lakini nyanya hizo
pendwa ndizo zinashambuliwa sana na ugonjwa mnyauko.
“Mimi niwaombe sana wenzetu wa
makampuni ya uzalishaji wa mbegu yaliyo hapa kutafuta uwezekano wa kuzalisha
mbegu hizo hizo pendwa sokoni lakini ziwe na uwezo wa kukinzana na ugonjwa wa
mnyauko wa nyanya au watusaidia kuzalisha mbegu nyingine mpya ili tuondokane na
changamoto hii ambayo inaleta kilio kwetu sisi kama wakulima” , alieleza bw. Khalid.
Kwa upande wake Afisa Kilimo kata
ya Mlali bw. Conrad Isack amesema kuna mbegu ambazo zipo kwenye majaribio
ambazo zimeonekana kufanya vizuri sana shambani na zina uwezo wa kuvumilia
ugonjwa wa mnyauko lakini bado hazijasajiliwa hivyo akaomba watafiti wa mradi
huo kwa kushirikiana na makampuni ya mbegu inayoizalisha mbegu hiyo kusaidia
iingie sokoni.
“Mbegu hii kwa ugonjwa wa mnyauko
inafanya vizuri sana lakini pili tunda lake linahimili kusafirishwa umbali
mrefu, tatu mchuzi wake ni rojo mchuzi mzito lakini nne inavutia na wakulima
wanahitaji mbegu hiyo walime maana imefanyiwa majaribio kwa miaka mingi lakini
sokoni haipo haijasajiliwa hivyo tunawaomba muharakishe usajili wa mbegu hiyo
inaweza kuwa mkombozi kwa wakulima wa zao la nyanya nchini”, alisema Bw.
Conrad.
Akitoa ufafanuzi kuhusu ombi hilo
Angus Hamilton kutoka kampuni ya Sakata Seed ya Kenya amesema kuwa mbegu hiyo
tayari ipo sokoni nchini Kenya wakulima wanailima hivyo bado wanafuatilia
taratibu za mbegu hiyo pia kusajiliwa nchni Tanzania.
Amesema suala la uzalishaji wa
mbegu mpya moja ya nyanya inaweza kuchukua miaka zaidi ya kumi ili kupata mbegu
yenye sifa wanazozihitaji wakulima na kazi hizo bado zinaendelea hivyo
waendelee kutumia zilizopo kwa sasa kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa
kilimo kwenye maeneo yao.
“Ukiona tumeleta mbegu mpya ya
nyanya sio kwamba tumefanya jana bali ni kazi pengine iliyofanywa na baba zetu
na kazi tunazofanya leo za uzalishaji wa mbegu bora ni kwa ajili ya watoto
wetu, sisi kampuni yetu kila mwaka tunaleta mbegu kwa ajili ya majaribio na
tunaendelea na kazi bila kuchoka ndiyo maana
hapa kwenye majaribio haya ya SUA –Fair Planet tuna aina 8 ya mbegu mpya
za nyanya, Kabichi aina tano za pilipili hoho na maboga na tunaendelea kuleta” ,
alisema Hamilton.
Kwa upande wake Wiliam Hilonga
kutoka Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania TOSCI amesema usajili wa
mbegu yoyote nchini una taratibu kadhaa ambazo lazima zifuatwe ili kujiridhisha
na ubora wake kabla ya kuanza kutumika nchini.
“Sisi kama Taasisi tunachoangalia
zaidi ni kupata mbegu ambayo inakwenda kuwa suluhisho la changamoto za wakulima
iwe ni kukinzana na wadudu na magonjwa au uwezo wake wa uzalishaji au vyote kwa
pamoja kwa kuwa kila mbegu inayozalishwa inakuwa na lengo na sifa maalumu kwa
wakulima hivyo nitafuatilia kuona sababu za kuchelewa kusajiliwa kwa mbegu zilizotajwa
kuwa sasa zinatumiwa na wakulima nchini Kenya”, alifafanua Hilonga.
Naye mtaalamu kutoka kampuni ya
Bayer Feminis Bw. Paul Kilenga amewataka wakulima kufanya uchaguzi wa aina ya
nyanya ya kulima kwa kuangalia mazingira ya ustawi wa nyanya wakati watafiti
wakiendelea kutafuta mbegu bora zinazojibu mahitaji yao.
“Hivi sasa mpango mkubwa uliopo
katika msimu ujao wa kilimo inatarajiwa kuingia mbegu mbili ambazo zina uwezo
wa kuhimili magonjwa hayo pamoja na kuwezesha mkulima kuchuma michumo hadi 16
nyanya kubwa pekee bila chenga hivyo kwa mbegu hiyo tunaamini wakulima wetu
wataweza kupata faida maradufu na kujikwamua kutoka kwenye wimbi la umasikini”, alisema Bw. Kilenga.
Amesema mazingira ya sasa
yanaonesha kuwa maeneo ya kilimo yanapungua na gharama ni kubwa hivyo wakulima
wanahitaji kulima kwenye maeneo madogo lakini waweze kupata mavuno makubwa kwa
maana ya kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji na tayari Taasisi ya
Uthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) wameshatoa chetu cha usajili.
Shamba darasa hili na maonesho limeandaliwa
na Mradi wa SUA –Fair Planet na kuwakutanisha wakulima, Maafisa kilimo na
Ugani, Makampuni ya uzalishaji na usambazaji wa mbegu na wadau wengine wa mazao
ya bustani na kilimo kwa ujumla zaidi ya 100.
Mkulima maarufu wa nyanya mkoani Morogoro bw. Khalid Gumbo akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake. |
Afisa Kilimo kata ya Mlali bw. Conrad Isack akitoa uzoefu wake mbele ya wadau. |
Wiliam Hilonga kutoka Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania TOSCI akifafanua kwa wadau kuhusu hoja zilizoibuliwa kuhusu usajili wa mbegu. |
Bw. Angus Hamilton kutoka kampuni ya Sakata Seed ya Kenya akitoa ufafanuzi kuhusu aina ya mbegu zilizopendwa. |
Mtaalamu kutoka kampuni ya Bayer Feminis Bw. Paul Kilenga akieleza hoja zilizowasilishwa kuhusu kampuni yao. |
Wadau wakifuatilia hoja mbalimbali majadiliano. |
Mratibu wa Mradi huo kwa upande wa Fair Planet kutoka Izrael Bi.Rinat Kaplan akitoa shukrani kwa wadau waliofanikisha shughuli hiyo. |
0 Comments