SUAMEDIA

SUA - Fair Planet yapongezwa kwa kuwajengea uwezo wadau wa kilimo kwenye kilimo cha mazao ya bustani Morogoro.

 Na: Calvin Gwabara – Morogoro.

Wadau wa Kilimo Wilaya ya Mvomero na Manispaa ya Morogoro wameipongeza SUA kupitia mradi wa Fair Planet kwa kuwajengea uwezo wakulima na wataalamu wa kilimo cha Mbogamboga na matunda na kuwakutanisha na wazalishaji wa mbegu hizo ili kueleza changamoto za mbegu wanazozalisha na faida zake.

Picha ya pamoja ya wataalamu wa Kilimo wa Wilaa ya Mvomero, Manispaa ya Morogoro, wadau wengine toka sekta binafsi  na Makampuni ya uzalishaji na usambazaji wa Mbegu.

Wakizungumza kwenye maonesho ya mashamba darasa ya majaribio ya mbegu mbalimbali za mbogamboga kwenye shamba la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Mjini Morogoro na kuwakutanisha wataalamu hao zaidi ya 100 wanaoshiriki kwenye majaribio na mashamba darasa kwenye kata mbalimbali za wilaya ya Mvomero, Kaimu Afisa Kilimo, Mifugo na uvuvi wa wilaya hiyo Bi. Blandina Marijani amesema wanajivunia kazi kubwa iliyofanywa katika kipindi chote cha mradi huo.

“Tunaishukuru SUA na Fair Planet kwa kazi kubwa waliyoifanya kwenye wilaya yetu kwa kutusaidia kutoa huduma za ugani kwenye kata nane na vijiji 11 ambako kote kuna mashamba darasa ambayo hakika ni mazuri sana na yamewekwa barabarani kiasi kwamba kila mkulima anayepita anaona na kujifunza” , alieleza Bi. Blandina.

Aliongeza “Kingine tunachowashukuru ni kutusaidia kutoa mafunzo kwa maafisa ugani wetu ambapo hata mimi binafsi nimenufaika nayo kwa kujifunza mambo mengi hasa kuhusu kilimo cha nyanya hivyo ni jambo kubwa maana sisi kama Serikali tunashirikiana na sekta binafsi katika kutoa huduma za ugani kwa wakulima na wataalamu”.

Amesema kitendo cha Mradi huo kuwakutanisha na makampuni ya uzalishaji wa mbegu bora za nyanya kimewapa nafasi ya kuzungumza nao kuhusu mbegu wanazozalisha na changamoto ya upatikanaji wake kwa kuwa maeneo mengi wakulima wanatumia mbegu za kukamua ambazo zinarudisha nyuma tija kila mwaka.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Mazao na Bustani Dkt. Richard Madege ambaye pia ni mmoja wa viongozi wa mradi huo kutoka SUA amesema ushirikiano huo kati ya SUA na Mradi wa Fair planet kutoka nchini Izrael kupitia shughuli zake unakazia malengo makuu ya Chuo ya kufanya utafiti na kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu kwa jamii.

“Kitu cha kipekee kabisa ambacho mradi huu unafanya ni kuunganisha jamii kwa kuwakutanisha na kufanya kazi pamoja kati ya watafiti kutoka SUA, wataalamu wa kilimo kutoa halmashauri, wakulima na makampuni ya uzalishaji wa mbegu na hiyo ni ushara ya kuonesha kuwa SUA haijajifungia kwenye mipaka yake bali inatoka na kuwafikia wadau wake hadi ngazi za chini kuhakikisha tunabadilisha maisha ya watu” , alisema Dkt. Madege.

Hivyo amesema Idara ya Sayansi ya Mazao na Bustani inajivumia mradi huo na siku hiyo ya mkulima shambani inakamilisha mpango mzima wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma kukaa pamoja na kujifunza kutoka kwa kila upande ili kupata majibu ya changamoto za wakulima nchini.

Naye Mratibu wa Mradi huo kwa upande wa Fair Planet kutoka Izrael Bi.Rinat Kaplan amesema mradi huo una mihimili miwili ambayo mmoja ni upande wa utafiti ambapo mbegu mbalimbali zinafanyiwa majaribio kuona uzuri na changamoto zake na zile nzuri kuzipeka kwa wakulima lakini mhimili mwingine ambao ni muhimu ni ule wa kupeleka maarifa hayo kwa wakulima kupitia mafunzo mbalimbali kitu ambacho mara nyingi watu wa utafiti hawakutani na watu wa mafunzo na jamii.

“Mara nyingi makampuni ya mbegu hayapati nafasi ya kukutana na maafisa ugani kueleza kuhusu mbegu zao lakini ni muhimu nao waweze kujua namna ya maarifa hayo yanavyokusanywa mwisho wa siku yanavyowafikia wakulima hivyo siku ya leo ni kuwakutanisha wote pamoja kusikia mahitaji ya kila mmoja na kubadilishana maarifa”,  alieleza Bi. Rinat.

Aliongeza” Wakulima wanaweza kupata nafasi ya kueleza wanahitaji aina gani ya sifa za mbegu na kwa sababu zipi ili makampuni ya uzalishaji wa mbegu waweze kuzalisha au kuboresha mbegu zao ziendane na mahitaji ya wakulima na soko lakini pia maafisa ugani kuweza kujua mbinu zilizotumika kwenye mashamba darasa hayo zinavyoweza kusaidia kuongeza tija kwa mkulima”.

Mradi wa Fair Planet ulianza kazi zake mwaka 2019 nchini Tanzania na unafanya kazi pia nchini Ethiopia kwa muda wa miaka 8 sasa na una vituo vya mafunzo kwenye kanda tatu za kilimo zikiwa na mashamba darasa ya mfano 2300 na kuhusisha zaidi ya wakulima wadogo 75,000 na kunufaisha zaidi ya watu wa kujitolea 160.


Kaimu Afisa Kilimo, Mifugo na uvuvi wa wilaya ya Mvomero  Bi. Blandina Marijani akitoa salamu za wilaya ya Mvomero.

 

Dkt. Richard Madege Akitoa salamu za Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Mazao na Bustani  kwenye ufunguzi wa siku ya maonesho na mafunzo shambani.

Mratibu wa Mradi huo kwa upande wa Fair Planet kutoka Izrael Bi.Rinat Kaplan akitoa salamu za Fair Planet.

Baadhi ya wataalamu wa kilimo walioshiriki kwenye siku hiyo ya maonesho na mafunzo shambani iliyofanyika SUA.

MATUKIO KATIKA PICHA WASHIRIKI WAKITEMBELEA SHAMBA LA MAFUNZO NA KUPATA MAELEZO.

















Post a Comment

0 Comments