SUAMEDIA

SUA yajenga na kukarabati majengo yatakayogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 41

 

Na: Tatyana Celestine

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimesaini mikataba ya ujenzi ya  majengo tisa na kufanya ukarabati katika maeneo mbalimbali ikiwa ni utekelezaji wa  azma ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa ufadhili wa Benki ya Dunia  kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ili  kuleta mageuzi ya kiuchumi Tanzania.

                                    

Katika utiaji saini huo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amesema mradi huo unaotarajiwa kutumia miezi 18 kukamilika utaanza mara baada ya kutia saini ambapo utagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 41 ambapo majengo matano yatajengwa katika Kampasi ya Edward Moringe, mawili Kampasi ya Solomoni Mahlangu na mengine mawili yatajengwa katika Kampasi ya Mizengo Pinda mkoani Katavi.

                                       

Naye mwakilishi wa Katibu wa HEET Taifa Dkt. Kennedy Hosea, Kiongozi wa Majenzi  Mradi wa HEET Taifa Mhandisi Hanington Kagiraki ameiomba Jumuiya ya Chuo kuwapa ushirikiano wakandalasi ili kuwezesha kufanya kazi kikamilifu,wanatarajia kupokea majengo yenye ubora, hadhi iliokusudiwa na kwa wakati kabla ya mradi kufungwa sambamba na kuzingatia gharama za mradi zisizidi zile ambazo zimepangwa, mawanda ya mradi kubaki yaleyale kama yaliyoainishwa katika mkataba.

                                  

Aidha Mhandisi Kagiraki amesema majengo hayo yakabidhiwe kwa kuta, sakafu lakini pia yawe na vifaa vyote, kama darasa liwe na vifaa vyake kwakuwa wanapaswa kutumia pesa kama inavyotakikana kwani mradi huo ni tofauti na miradi mingine hivyo wakandalasi wanatakiwa kuwasilisha hati ya malipo ya awali (Advance Payment Guarantee) ili kufanyiwa malipo ya asilimia 20 ya shilingi bilioni 41.1 haraka ili waweze kutekeleza mradi huo kwa wakati.

Ameongeza kuwa mradi wa HEET unatekelezwa katika vyuo vikuu nchini lakini wengi hawajafikia hatua ya kutia saini hivyo SUA ina kazi moja kwasasa ya kusimamia kikamilifu utekelezaji huo kwani wakandalasi wanatakiwa kutekeleza ujenzi wa majengo hayo kwa ubora na ufanisi kama ilivyokusudiwa.

Akizungumza mara baada ya utiaji saini wa ujenzi wa majengo hayo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima ambaye ni mgeni rasmi katika hafla hiyo amesema yeye kwa kushuhudia mradi huo ni ishara kuona mageuzi ya kiuchumi yanaendelea kufanyika kupitia chuo hicho ikiwa ni makusudi na nia ya dhati ya Serikali kuendelea kufanya mambo makubwa  SUA kama walivyoanza ujenzi wa Samia Complex  kwa kujenga jengo linalochukua watu 3000 kwa wakati mmoja na sasa majengo hayo tisa.

                                

Aidha amepongeza Menejimenti ya Chuo kwa kuweka Mkandalasi mzawa katika utekelezaji wa mradi huo na kusema kwa kupitia mkandalasi huyo akawe picha Tanzania kwa kuonesha wakandalasi wazawa wanaweza kufanya kazi kwa kuzingatia ubora na muda uliopangwa na kuahidi kupita mara kwa mara kuangalia muenendo wa mradi huo ingawa hana mashaka wa usimamizi wa Menejiment ya Chuo cha SUA kama ilivyokuwa katika miradi iliyopita iliyotoa matokeo mazuri.

                                        

Mhe. Malima Ameongeza kuwa Rais Samia amekitaka Chuo hicho kikawe sehemu ya kimataifa kwa masuala ya kilimo hivyo hadhi yake iendane na majengo yaliyo bora na elimu bora ya kilimo kwani ni ndoto yake pia kama Mkuu wa Mkoa kwa kuwa anaamini kila kitu kitakuwa kizuri mara baada ya kikamilika.

Mkuu wa Mkoa huyo amebainisha ile ndoto ya mabadiliko ya kilimo nchini itaanzia Morogoro na kila mmoja ataiga kupitia mkoa huo kwani anaamini ndoto hiyo inawezekana kutimia kwa kupitia SUA hivyo wanatakiwa kushirikiana na ofisi yake ili kufanikisha ndoto hiyo kuwa kweli kwakuwa huu ni muda muafaka kwa kuleta maendeleo ya kilimo ambapo serikali inaunga mkono.

Aidha amesema yeye kama Mkuu wa Mkoa amekwishazungumza na Benki ya NMB na kuwataka SUA kushirikiana nao kwani wako tayari kutoa fedha katika kukuza kilimo mkoani hapo kutokana mkoa huo unazalisha mazao mbalimbali ikiwemo Karafuu, Parachichi, Chikichi, Kakao na Kahawa hivyo endapo SUA wataamua wataweza kukuza uchumi wa mkoa huo kupitia kilimo.

                                         

Ujenzi na ukarabati huo unatekelezwa na wakandalasi watatu ambao wawili ni kutoka China Jiangxi Peng wa Kampuni ya Chan International, Li Man Chaw wa Kampuni ya Shanpong Hi Speed Jian na kutoka Tanzania kutoka Kampuni ya WCEC Limited.

BOFYA HAPA CHINI KUFUATILIA MATUKIO NA PICHA  MRADI WA HEET-SUA

https://heetproject.pixieset.com/utiajisainiwaukarabatiwamkatabawaujenziwamajengosuakupitiaheet/

                                    



                                










 

 

 KATIKA VIDEO

Post a Comment

0 Comments