SUAMEDIA

Wakulima wa nyanya waomba watafiti kuboreshwa na kuzalishwa mbegu mpya zinazovumilia ugonjwa wa mnyauko.

 Na: Calvin Gwabara – Morogoro.

Wakulima wa zao la Nyanya mkoani Morogoro wamewataka wazalishaji na wasambazaji wa mbegu bora za nyanya nchini kuleta mbegu mpya au kuziboresha mbegu bora zilizopo sokoni ambazo zinashambuliwa sana na ugonjwa wa mnyauko na kuathiri tija kwa wakulima wa zao hilo.

Wadau wa kilimo Wilaya ya Mvomero na Manispaa ya Morogoro wakiangalia shamba darasa la mradi wa SUA - Fair Planet.

Wito huo umetolewa na Wakulima na Maafisa ugani kutoka Wilaya ya Mvomero na Morogoro wakati wakizungumza na makampuni ya uzalishaji na usambazaji wa mbego za Nyanya mara baada ya kuhitimisha zoezi la kutembelea mashamba darasa ya mazao ya bustani hususani nyanya yanayofanyiwa majaribio ya mbegu mbalimbali za bustani chini ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kushirikiana na Mradi wa Fair Planet kutoka nchini Izrael.

Akitoa uzoefu wake Mkulima maarufu wa nyanya mkoani Morogoro bw.  Khalid Gumbo amesema wao wanalima nyanya kutokana na uhitaji wa soko na soko linataka nyanya ambazo zina ganda gumu linalowezesha nyanya kukaa muda mrefu sokoni bila kuharibika lakini nyanya hizo pendwa ndizo zinashambuliwa sana na ugonjwa mnyauko.

“Mimi niwaombe sana wenzetu wa makampuni ya uzalishaji wa mbegu yaliyo hapa kutafuta uwezekano wa kuzalisha mbegu hizo hizo pendwa sokoni lakini ziwe na uwezo wa kukinzana na ugonjwa wa mnyauko wa nyanya au watusaidia kuzalisha mbegu nyingine mpya ili tuondokane na changamoto hii ambayo inaleta kilio kwetu sisi kama wakulima” , alieleza bw.  Khalid.

Kwa upande wake Afisa Kilimo kata ya Mlali bw. Conrad Isack amesema kuna mbegu ambazo zipo kwenye majaribio ambazo zimeonekana kufanya vizuri sana shambani na zina uwezo wa kuvumilia ugonjwa wa mnyauko lakini bado hazijasajiliwa hivyo akaomba watafiti wa mradi huo kwa kushirikiana na makampuni ya mbegu inayoizalisha mbegu hiyo kusaidia iingie sokoni.

“Mbegu hii kwa ugonjwa wa mnyauko inafanya vizuri sana lakini pili tunda lake linahimili kusafirishwa umbali mrefu, tatu mchuzi wake ni rojo mchuzi mzito lakini nne inavutia na wakulima wanahitaji mbegu hiyo walime maana imefanyiwa majaribio kwa miaka mingi lakini sokoni haipo haijasajiliwa hivyo tunawaomba muharakishe usajili wa mbegu hiyo inaweza kuwa mkombozi kwa wakulima wa zao la nyanya nchini”, alisema Bw. Conrad.

Akitoa ufafanuzi kuhusu ombi hilo Angus Hamilton kutoka kampuni ya Sakata Seed ya Kenya amesema kuwa mbegu hiyo tayari ipo sokoni nchini Kenya wakulima wanailima hivyo bado wanafuatilia taratibu za mbegu hiyo pia kusajiliwa nchni Tanzania.

Amesema suala la uzalishaji wa mbegu mpya moja ya nyanya inaweza kuchukua miaka zaidi ya kumi ili kupata mbegu yenye sifa wanazozihitaji wakulima na kazi hizo bado zinaendelea hivyo waendelee kutumia zilizopo kwa sasa kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa kilimo kwenye maeneo yao.

“Ukiona tumeleta mbegu mpya ya nyanya sio kwamba tumefanya jana bali ni kazi pengine iliyofanywa na baba zetu na kazi tunazofanya leo za uzalishaji wa mbegu bora ni kwa ajili ya watoto wetu, sisi kampuni yetu kila mwaka tunaleta mbegu kwa ajili ya majaribio na tunaendelea na kazi bila kuchoka ndiyo maana  hapa kwenye majaribio haya ya SUA –Fair Planet tuna aina 8 ya mbegu mpya za nyanya, Kabichi aina tano za pilipili hoho na maboga na tunaendelea kuleta” , alisema Hamilton.

Kwa upande wake Wiliam Hilonga kutoka Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania TOSCI amesema usajili wa mbegu yoyote nchini una taratibu kadhaa ambazo lazima zifuatwe ili kujiridhisha na ubora wake kabla ya kuanza kutumika nchini.

“Sisi kama Taasisi tunachoangalia zaidi ni kupata mbegu ambayo inakwenda kuwa suluhisho la changamoto za wakulima iwe ni kukinzana na wadudu na magonjwa au uwezo wake wa uzalishaji au vyote kwa pamoja kwa kuwa kila mbegu inayozalishwa inakuwa na lengo na sifa maalumu kwa wakulima hivyo nitafuatilia kuona sababu za kuchelewa kusajiliwa kwa mbegu zilizotajwa kuwa sasa zinatumiwa na wakulima nchini Kenya”, alifafanua Hilonga.

Naye mtaalamu kutoka kampuni ya Bayer Feminis Bw. Paul Kilenga amewataka wakulima kufanya uchaguzi wa aina ya nyanya ya kulima kwa kuangalia mazingira ya ustawi wa nyanya wakati watafiti wakiendelea kutafuta mbegu bora zinazojibu mahitaji yao.

“Hivi sasa mpango mkubwa uliopo katika msimu ujao wa kilimo inatarajiwa kuingia mbegu mbili ambazo zina uwezo wa kuhimili magonjwa hayo pamoja na kuwezesha mkulima kuchuma michumo hadi 16 nyanya kubwa pekee bila chenga hivyo kwa mbegu hiyo tunaamini wakulima wetu wataweza kupata faida maradufu na kujikwamua kutoka kwenye wimbi la umasikini”,  alisema Bw. Kilenga.

Amesema mazingira ya sasa yanaonesha kuwa maeneo ya kilimo yanapungua na gharama ni kubwa hivyo wakulima wanahitaji kulima kwenye maeneo madogo lakini waweze kupata mavuno makubwa kwa maana ya kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji na tayari Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) wameshatoa chetu cha usajili.

Shamba darasa hili na maonesho limeandaliwa na Mradi wa SUA –Fair Planet na kuwakutanisha wakulima, Maafisa kilimo na Ugani, Makampuni ya uzalishaji na usambazaji wa mbegu na wadau wengine wa mazao ya bustani na kilimo kwa ujumla zaidi ya 100.


Mkulima maarufu wa nyanya mkoani Morogoro bw.  Khalid Gumbo akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake.

Afisa Kilimo kata ya Mlali bw. Conrad Isack akitoa uzoefu wake mbele ya wadau.

Wiliam Hilonga kutoka Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania TOSCI akifafanua kwa wadau kuhusu hoja zilizoibuliwa kuhusu usajili wa mbegu.


Bw. Angus Hamilton kutoka kampuni ya Sakata Seed ya Kenya akitoa ufafanuzi kuhusu aina ya mbegu zilizopendwa.

Mtaalamu kutoka kampuni ya Bayer Feminis Bw. Paul Kilenga akieleza hoja zilizowasilishwa kuhusu kampuni yao. 



Wadau wakifuatilia hoja mbalimbali majadiliano.


Mratibu wa Mradi huo kwa upande wa Fair Planet kutoka Izrael Bi.Rinat Kaplan akitoa shukrani kwa wadau waliofanikisha shughuli hiyo.

Post a Comment

0 Comments