Na: Eden Bahati
Mkuu wa
Mkoa wa Morogoro Adam Malima amewataka Wataalamu wa Misitu kutoka Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA) kuhamasisha utekelezaji wa utunzaji na uendelezaji wa
misitu nchini kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye.
Amebainisha
hayo Oktoba 3, 2024 wakati wa kufunga Maadhimisho ya Miaka 50 ya kuanzishwa kwa
Kitivo cha Mafunzo ya Misitu kilichopo SUA ambapo amesema kitu wanachotakiwa
kukifanya ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuisadia kupata uelewa wa umuhimu wa uhifadhi wa
Misitu katika maeneo yote kwa ajili ya kukiwezesha kizazi kijacho kuja
kunufaika na misitu na mazingira kiujumla.
Aidha
Malima amesema Wataalamu kutoka SUA wanapaswa kuifahamisha jamii athari
zinazotokea kutokana na uharibifu wa misitu ambao kwa kiasi kikubwa
unasababishwa na shughuli za binadamu ikiwemo kuchoma mkaa, kukata kuni na
shughuli za kilimo hasa maeneo ya pembezoni mwa miji.
Kwa
upande wake Bi. Metrida Kaijage Mtaalamu wa Sheria kutoka SUA amesema
wataalamu wana wajibu wa kutunga miswada na kupeleka kwa Serikali ili
kuhamasisha matumizi sahihi ya rasilimali misitu lakini pia amezitaka Taasisi
kama SUA kutafuta wadau ambao watashirikiana nao katika uratibu wa uhifadhi
misitu.
“Natumaini ni yangu kutoka kwa wataalamu kutoka SUA mtaendelea kufanya
tafiti zenye tija kuhusiana na misitu ikiwemo njia sahihi za kutatua changamoto
za kidunia ambazo zinaathiri misitu na mazao yake pamoja na tafiti za kisayansi
za misitu”, amesema Bi. Metrida Kaijage.
Naye
Prof. August Temu ambaye pia ni Mtaalamu mbobevu wa Misitu kutoka SUA amesema anaiona
Tanzania ikiendelea kufanya vizuri katika utunzaji wa Misitu kwani SUA
inaendelea kuzalisha wataalam wengi wa misitu ambao watazidi kuwa vinara wa
utunzaji Misitu na rasilimali zake kwa manufaa makubwa ya jamii na kizazi cha
kesho.
“Miaka 50
ijayo naiona Tanzania ikifikia hatua ya nchi kama Finland na China ambazo
zinatumia vizuri mazao ya misitu kwani katika nchi hizo kila zao la msitu lina
matumizi katika viwanda vya uzalishaji
malighafi, ambazo zinatumika kuinua uchumi wa nchi hivvo naamini Tanzania
itafikia hatua hiyo kama endapo tu watu wataweza kutunza misitu kikamilifu”,
amesema Prof. Temu
Kwaa upande wake Agnes Sirima ambae ni Rasi wa ndaki ya Misitu Wanyamapori na Utalii, amesema ndaki hiyo imedhamiria kuendeleza kituo cha umahiri katika taaluma ya misitu ambacho kipo chini ya SUA chenye lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusiana na Misitu lakini pia kwa ajili ya kujiendeleza kwa Wafanyakazi ambao wapo katika sekta ya Misitu.
Aidha ameongeza kuwa wanatarajia kuongeza ushirikiano kati ya SUA na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake zote ili kuendeleza taaluma ya misitu nchini lakini pia kuongeza wigo mpana wa mafunzo kwa vitendo kwa Wanafunzi pamoja na kuhakikisha tafiti zinazofanywa SUA zinaifikia jamii na kuboresha sera za uendeshaji sekta ya misitu nchini.
0 Comments