SUAMEDIA

Wanafunzi wenye mahitaji maalum SUA wapatiwa miguu bandia kupitia Mradi wa HEET

 

Na: Tatyana Celestine, Dar es Salaam     

Wanafunzi wenye mahitaji maalum kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wamenufaika na Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa kuwapatia miguu bandia ili kuwarahisishia kufanya shughuli zao za kila siku hasa wawapo katika mazingira ya chuo katika kuitafuta elimu.

                                

Akizungumza na SUAMEDIA Mratibu wa Elimu Jumuishi na Mahitaji Maalum SUA chini ya Mradi wa HEET Dkt. Thabita Lupeja amekishukuru Menejimenti ya Chuo cha SUA kwa kuwezesha mradi huo kufika chuoni hapo ambapo mbali na kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunza, kuboresha mitaala, kuwajengea uwezo wa kitaaluma watumishi lakini haujawasahau watu wenye mahitaji maalum kwa kuweka  mazingira wezeshi katika utendaji wa kazi za kila siku.

Dkt. Lupeja ameeleza kuwa kutokana na sababu mbalimbali za ulemavu wa miguu, wanafunzi hao wameonekana wakiwa na matumaini mapya na kukishukuru Chuo Kikuu cha Sokoine kwa kuwajali bila kujali umri, jinsi , kipato na hata mazingira waliyotoka na hivyo kuwafanya wao kuona mwanga wa maisha tena tofauti na awali ambapo walikuwa na hali ya kukata tamaa na kutengwa.

Akizungumzia wanafunzi ambao wapo kwenye hatua za mwisho kupatiwa miguu bandia  Mratibu huyo amesema wanafunzi hao wamegawanyika katika makundi mawili wapo wanaohitaji mguu mmoja na wale wenye uhitaji wa miguu yote miwili hivyo inatia faraja kuona hospitali ya CCBRT inajitoa kuwashughulikia kwa ukaribu na hatimaye wamefikia hatua ya mazoezi ya kutembelea miguu hiyo ili waweze kuitumia rasmi kama kifaa saidizi katika kutembea.

                            

Kwa upande wa Mtaalamu wa Viungo na Vifaa Tiba Saidizi wa Hospitali ya CCBRT Dkt. Evance Maimu amesema vijana hao ni rahisi kuweza kufuzu mazoezi kwa haraka kulingana na umri wao kwa sasa wanapimwa miguu na kufanya mazoezi ambapo ndani ya wiki moja wataweza kutembea wenyewe kwa kutumia miguu bandia hivyo Chuo kizidi kuwasaidia watu wenye uhitaji wao wapo tayari kuwapatia huduma.

                                

Naye Mtaalamu wa Viungo na Vifaa Tiba Saidizi wa Hospitali ya CCBRT Dkt. Gasper Shirima amekipongeza Chuo Kikuu cha SUA kwa kuwapatia vijana wao vifaa tiba, kwa kufanya hivyo wamesaidia kukuza uchumi wa nchi kwani huwezi kukuza uchumi wa nchi kama huwezi kufanya kazi hivyo vifaa hivyo vitawawezesha katika shughuli zao za uzalishaji. 

                                

Alipotakiwa kuelezea ni kwa namna gani wanafunzi hao wanatakiwa kupokelewa katika jamii mara baada ya kupatiwa matibabu hayo Muuguzi Mwandaizi kutoka Kurugenzi ya Huduma za Hospitali SUA Bi Christina Semwenda amewaasa wanajamii  kutowanyanyapaa watu wenye mahitaji maalum ili kujenga jamii jumuishi na kuwahakikishia ushirikiano pamoja na kuitaka jumuiya ya SUA kuwajali na kuwapa kipaumbele hasa katika kupata huduma muhimu kama malazi chuoni hapo.

 


 


Post a Comment

0 Comments