SUAMEDIA

Wanafunzi zaidi ya elfu 22 wameomba kujiunga SUA mwaka wa masomo 2024

 Na Gerald Lwomile

Wanafunzi zaidi ya elfu 22 kutoka ndani na nje ya nchi wameomba kujiunga na masomo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa mwaka wa masomo 2024 huku nafasi zikiwa ni elfu 7 tu.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda akizungumza katika Mkutano wa Majalisi Watendaji Wakuu wa Mashirika (Picha zote na Adam Ramadhan)

Akizungumza Octoba 15, 2024 katika Mkutano wa Pili wa Mwaka wa Majilisi wa SUA ambao unahusisha Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Serikali na yasiyo ya Serikali, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda amesema idadi hiyo inaakisi ubora wa Chuo hicho unaondelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Prof. Chibunda amesema katika kuhakikisha SUA inaendelea kutoa wahitimu wanaoweza kuajiriwa na kujiajiri imeendelea kuboresha miundombinu ya kufundisha ikiwa ni pamoja na kufanya mafunzo kwa vitendo ambapo hivi sasa Chuo kimenunua gari ya kuchimba visima kwa zaidi ya shilingi milioni 200 na kuishukuru Serikali kwa kuwezesha mpango huo.

“SUA ni Chuo pekee kinachofundisha Uhandisi wa Umwagiliaji hivyo ingekuwa ajabu Mhandisi anatoka SUA hata gari tu la kuchimba visima hajui linafanyaje kazi………..., SUA siyo mahali pa kuigiza kama mwanafunzi amekuja kusoma mfano matibabu ya Wanyama kama ni ng’ombe basi ataangushwa kweli na kutibiwa ili apone” amesema Prof. Chibunda.

Wakitoa maoni yao katika Mkutano huo Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Serikali na yasiyo ya Serikali waliosoma SUA wamesema wamefurahishwa na maendeleo makubwa yaliyofikiwa na SUA na kukitaka Chuo hicho kuhakikisha hakirudi nyuma.

Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Serikali na yasiyo ya Serikali wakisikilza maeleo kutoka kwa Bw. Alpha Mtakwa wa Idara ya Shamba Darasa SUA

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) Prof. Madundo Mtambo ambaye pia ni amesoma SUA amesema Chuo hicho kiangalie uwezekano wa kuhakikisha kinawatembelea Watendaji hao Wakuu na hasa katika Sekta Binafsi ili kuona hatua, changamoto na namna wanaweza kuwasaidia katika kuhakikisha wanafikia malengo yao.

Akizungumza katika mkutano huo Mtendaji Mkuu Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Dkt. Pius Mwambene amekipa changamoto Chuo hicho kuhakikisha kinafanya tafiti na kuzalisha mbengu bora za wanyama wakiwemo Ng’ombe kwani mahitaji ni mkubwa, ameongeza kuwa hivi sasa mfugaji akitaka mbegu bora ya Ng’ombe lazima uagize nje hivyo  ni vyema SUA ikajikita katika eneo hilo.

Naye Bw. Mabula Maganga Mkurugenzi kutoka Afya ya Mnyama amesema kuna changamoto kubwa kwa wahitimu SUA katika kupata mitaji na hivyo ni muhimu kwa SUA ikashiriki kikamilifu katika kutafuta njia bora za kuwezesha wahitimu wake wenye nia ya dhati katika upatikanaji wa mitaji kupitia kitengo chake cha Ubunifu.

Kwa upande wake Bw. Ziadi Rwamugira kutoka Kampuni ya Usambazaji wa Mbegu ya AGRINATURE amesema SUA iangalie uwezekano wa kuhakikisha tafiti zake na hasa zile za uzalishaji wa mbegu zinawafikiwa wazalishaji wa mbengu nchini ambao zaidi ya asilimia 29 ya wazalishaji hao ni kutoka SUA hivyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Uthibiti wa Mbegu TOSCI, SUA itakuwa imewawezesha wazalishaji hao na kuinufaisha jamii.

Akitoa maazimio ya Mkutano huo Katibu wa Majalisi SUA Prof. Jonathan Mbwambo amesema Chuo hicho kitajipanga kuhakikisha kinawafikiwa Watendaji hao Wakuu wa Mashirika na kujua ni namna gani kitashiriki katika kuhakikisha wanaendelea kupiga hatua katika shughuli zao za maendeleo.

Naye Kaimu Rais wa Majalisi SUA, Dkt. Raymond Salanga amesema SUA imekuwa inajisikia fahari kubwa kuona miongoni mwa Majalisi wanashika nafasi kubwa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni katika Taassisi na Mashirika ya Kiserikali lakini pia katika Makampuni na Mashirika yasiyo ya Kiserikali na inawapongeza  waliojiajiri katika Nyanja mbalimbali za kilimo na kuajiri wenzao.

Mkutano wa Pili wa Mwaka wa Majalisi SUA ambao unahusisha Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Kiserikali na yasiyo ya Kiserikali, umefanyika ikiwa ni siku moja kabla ya Mkutano wa Majalisi wote wa SUA unaofanyika Octoba 16, 2024 na kufuatiwa na Mahafali ya 44 ya Chuo hicho yanayofanyika Octoba 17, 2024.








Post a Comment

0 Comments