Na: Tatyana Celestine
Katika kuelekea Maafali ya 44,
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimetunuku Tuzo 228 kwa watafiti, wafanyakazi, na wanafunzi
waliofanya vizuri ambapo wanafunzi hao wamepata fursa ya kuajiriwa kupitia
Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) pamoja na kukaribishwa Benki kiongozi (CRDB) kufanya
mafunzo kwa vitendo.
Akizungumza baada ya kutunuku
tuzo hizo Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi. Cpyrian Luhemeja amesema
wanafunzi hao waliotunukiwa tuzo wanatakiwa kuhakikisha elimu waliyopata inaakisi
kile ambacho wamejifunza katika kutengeneza kizazi kijacho kitakachjitengenezea
ajira zao wenyewe na kufanya mabadiliko katika dunia kulingana na teknolojia.
Aidha Mhandisi Luhemeja amesisitiza tuzo zilizotolewa ni ishara ya kujituma na kufanya kazi kwa bidii hivyo amewataka wale ambao hawakupata tuzo kutambua katika maisha kuna kufaulu na kufeli ili kufanikiwa zaidi lazima waweze kufanya vizuri na hata wakifeli wasiogope kujaribu tena.
Akizungumzia ubora wa Tafiti za SUA Mhandisi Luhemeja amesema Chuo hicho kimekuwa kikifanya vizuri na kuonesha umahiri kila wakati ambao unasaidia kutatua matatizo katika dunia ya leo na kukitaka chuo cha SUA kuendelea kuwekeza zaidi katika utafiti na ufundishaji kukabiliana na akili mnemba (AI) kwani dunia inataka mtazamo ubadilike na ili kuchagiza ubora na ufundishaji kwa Chuo hicho, Ofisi ya Rais itandaa Tuzo za Makamu wa Rais (Vice President Award) kuanzia mwaka ujao.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Prof.
Rafael Chibunda amesema lengo la tuzo hizo ni kuongeza hamasa kwa wanafunzi na
wafanyakazi ili kuendelea kufanya vizuri katika kazi, masomo na uongozi ambapo SUA
kimeendelea kufanyia maboresho mitaala yao pamoja na kusimamia mafunzo kwa
vitendo ambayo kwasasa yamesaidia wanafunzi wao kupata ajira na kujiajiri.
Naye Kamishna wa Uhifadhi Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania ambaye pia ni muhitimu wa SUA Prof. Dos Santos Silayo amesema
wamekuwa wakiajiri wahitimu wa SUA kupitia Fani za Sayansi za Misitu,
Wanyamapori, Utalii na Mazingira, kwani hivi sasa chuo kimepiga hatua kwa
kuboresha ufundishaji na mafunzo wanayoyatoa kwa kuzingatia mabadiliko ya
sayansi na teknolojia.
Wakizungumzia tuzo ambazo wamepokea wahitimu watarajiwa wa Kozi ya Biyoteknolojia na Sayansi ya Maabara Bi.Daylight Mhongole na Bw. Karimu Muhara wamesema ukuaji wa teknolojia imekuwa fursa inawasaidia katika kusoma, tafiti lakini pia kujituma katika kila wanachokifanya hivyo wamewashauri wanafunzi wengine kutumia mafunzo kwa vitendo, teknolojia za kisasa kujitolea katika kazi ili kuwasaidia kuwa wanasayansi wakubwa na kutopishana na soko la ajira.
0 Comments