SUAMEDIA

Wanataaluma vyuo vikuu wekeni mikakati itayochochea maendeleo - Prof. Muhairwa

Na: Siwema  Malibiche.

Wanataaluma  nchini  wametakiwa kutumia mawazo yao vizuri  kwa kuja na mikakati mipya  itakayochochea maendeleo ya  elimu kwa kukosoa, kushauri  na kuboresha  ili kukuza  sekta   ya elimu  kwa  maslahi ya Taifa.


Naibu Makamu Mkuu  Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo upande wa Mipango, Utawala na Fedha Prof. Amandus Muhairwa akifungua kikao


Hayo yamebainishwa na Naibu Makamu Mkuu   Mipango, Utawala na Fedha wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Amandus Muhairwa wakati akifungua kikao cha wanataaluma wa elimu ya juu kutoka vyuo mbalimbali nchini kilichofanywa kwa siku mbili katika ukumbi wa ICE uliopo  ndani ya  kampasi ya Edward Moringe Mkoani Morogoro.

Prof. Muhaimrwa amesema anatarajia wanataaluma hao watajadili masuala mbalimbali ikiwemo maslahi ya wanataaluma,masuala ya viwango vya elimu na maendeleo ya sekta ya elimu kwa upana wake ili kuboresha mazingira ya kazi kwa wanataaluma hao.

Aidha, Prof. Muhairwa amefurahishwa na uamuzi wa uongozi wa jumuiya ya wanataaluma   wa elimu ya juu nchini  kufanya kikao chao  cha mwaka   katika Chuo Kikuu cha Sokoine  Kilimo  SUA  huku akiweka wazi kuwa anategemea kuwepo kwa mijadala mbalimbali  itakayoleta tija katika maendeleo ya elimu kwa kizazi kijacho  kutokana na kuwepo kwa wanatalauma bobezi na wazoefu.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Wajumuiya ya Wanataaluma Tanzania (ASAPUCT) Dkt. Julius Edward Mtwenya  amesema kuwa wamekutana SUA ili kufanya kikao cha Baraza linalojumuisha Jumuiya ya Wenyeviti kutoka katika vyuo vikuu mbalimbali nchini ikiwemo SUA na kutoa wito kwa wazazi nchini kuwekeza katika kuwapatia elimu bora watoto  huku akiwataka makundi  mbalimbali na wadau wa elimu kutoa ushirikiano katika kuhakikisha maendeleo katika sekta ya elimu nchini.

Adha, amesema kuwa waanataaluma wanatakiwa kuwekeza katika kufikiri ili kuleta mawazo mapya katika sekta ya elimu huku akiipongeza  Serikali, Mabaraza ya Wanataaluma na  wadau  wa elimu kwa kuendelea kujipanga na kuona jinsi gani wanaweza kutatua changamoto  ili kukuza sekta hiyo ya elimu nchini.

Naye, Katibu wa Shirikisho la Jumuiya ya Wanataaluma Tanzania Dkt. Maxmillian Chuchila amesema  kuwa  mkutano huo utaleta mijadala yenye maslahi mapana  itakayoleta tija  kwa maendeleo ya elimu kwa kizazi kijacho na kueleza kuwa amefurahi kuwa miongoni mwa washiriki katika kikao hicho na anaamini maendeleo katika sekta ya elimu yatapatikana .

Kwa upande wake , Mhadhili kutoka Chuo kikuu cha Ushirika Moshi  ambae  pia ni Katibu  kutoka Jumuiya ya Wataalamu Moshi Bi  Irene Biseko amesema kuwa kupitia mkutano huo kuna mambo mengi yataboresha  vyuoni kwa kuzingatia ongezeko la idadi ya wanafunzi wanao jiunga na elimu ya juu nchini na hasa kwa kuboresha mifumo na kuishauri serikali.







Post a Comment

0 Comments