SUAMEDIA

SUGECO, AGRA na USAID zawapa elimu wakulima kuzikabili changamoto katika kilimo

 Na: Ayoub Mwigune

Katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya kilimo nchini, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) kwa kushirikiana na mashirika mengine kama AGRA na SUGECO, wametekeleza mradi wa AIDI-I unaolenga katika kusaidia wakulima kupunguza gharama na kuimarisha uzalishaji wa mazao mbalimbali hasa ya  nafaka ili kuleta tija katika maendeleo.

Hayo yameelezwa na Bi. Irene Faustine ambae ni  Mratibu Mradi wa AIDI-I, wakati akizungumza na Wakulima wa Kata Saba (7) za Magadu, Boma, Mlimani, Mindu, Bigwa, Mzinga na Kauzeni  zilizopo Manisapaa ya Morogoro  ambao ni wanufaika wa Mradi huo.

Awali akielezea kuhusu lengo la mradi huo Bi. Irene amesema kuwa lengo kuu la mradi huo ni kupunguza athari za kuongezeka kwa gharama za uzalishaji zilizosababishwa na vita ya Urusi na Ukraine pamoja na  kuimarisha mfumo wa mbegu za mahindi na kunde huku pia ukijikita katika kutoa ushauri wa kilimo na  kuimarisha matumizi ya mbolea kwa wakulima na kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa kupitia mazao ya viungo.

Aidha Bi.Irene amesema ukosefu wa elimu ya kilimo biashara, mbegu bora, athari za mabadiliko ya tabia nchi na matumizi mabaya ya mbolea na viuatilifu ni miongoni mwa changamoto kwa wakulima wengi hivyo wamechagua maeneo hayo kwani yana wakulima wengi wa mahindi, maharagwe na mazao ya bustani yatawasaidia kuimarisha Uzalishaji wenye tija na kuzingatia usalama wa chakula.

Kwa upande wake Daud Joel ambaye ni miongoni wa wanufaika wa mradi huo ameshukuru USAID ,AGRA na SUGECO kwa kuwaletea mradi huo ambao umechangia kiasi kikubwa katika kuboresha shughuli zao za Kilimo kwani sasa wataweza kulima kisasa na kupata tija ambayo itaimarisha kipato chao pamoja na kukuza soko lao la mazao ya nafaka.

"Nimejifunza mengi mwanzo nilikuwa nalima bila kufuata tararibu za kilimo lakini baada ya wataalam kutupatia mafunzo haya nimenufaika kwa kupata ujuzi ambao umenisaidia katika mashamba yangu nawashukuru sana USAID ,AGRA na SUGECO naamini wataendelea kutoa mafunzo haya kwa watanzania wengi ili na wao waweze kunufaika na elimu hii" amesema Daud Joel.

Mradi wa AIDI unatekelezwa katika nchi tatu za Zambia Malawi pamoja na  Tanzania huku mkoa wa Morogoro wilaya 3 za Mvomero Malinyi na wilaya ya Morogoro zikinufaika na mead huo.

Post a Comment

0 Comments