SUAMEDIA

Kampuni ya Uzalishaji wa Sukari Bagamoyo yaipongeza SUA kwa kutoa wahitimu bora

 Na: Tatyana Celestine 

Uongozi wa Kampuni ya Uzalishaji wa Sukari Bagamoyo ulio chini ya Makampuni ya Bakhresa umekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kutoa wahitimu ambao wanaaminika kwa kiwango kikubwa katika mnyororo mzima wa uzalishaji wa bidhaa ya Sukari.

Akizungumza na Kitengo cha Mawasiliano na Masoko SUA, Meneja Rasilimali Watu wa Kiwanda cha Sukari Bagamoyo Bw. Habibu Issah amesema kuwa kiwanda chao chenye malengo ya kuzalisha tani Laki Moja kwa mwaka kimeridhishwa sana na ushirikiano kati yao na SUA kwani umekuwa na tija kwa kuwaletea wanafunzi wanaojifunza kwa vitendo ambao wanaongeza uzalishaji.



Bw. Issah amesema ukiufuatilia mnyororo mzima wa uzalishaji wa Sukuri kuanzia shambani, umwagiliaji, uwekaji wa mbolea, uvunaji na uchakatajiwa Sukari yenyewe, kumekuwa na wahitimu na wanafunzi wanaofanya mazoezi kwa vitendo na wamekuwa wakifanya kazi vizuri na sio mzigo katika utendaji wa kazi wao.

Aidha Meneja Rasilimali Watu huyo amesema kiwanda hicho ni cha kisasa na hata Teknolojia zake ni za kisasa lakini hakuna changamoto wanayopata wanapowapokea wanafunzi kutoka SUA kwani wanawapa mafunzo kidogo kama utaratibu wao na ni kwa sababu SUA imekuwa ikiwapatia nafasi ya kujifunza kwa vitendo mara kwa mara mafunzo ambayo yanawawezesha kujua teknolojia zinazoenda na wakati.

Kwa upande wake Bw. Saguti Ibrahimu ambaye ni Mtafiti Idara ya Kilimo katika Kiwanda cha Sukari Bagamoyo na pia ni mhitimu kutoa SUA amesema chuo hichi ni chuo bora kwa utoaji wa elimu kwani mafunzo waliyopata chuoni yametosha kuwafanya watimize majukumu yao pamoja na kuwepo kwa teknolojia ngeni za kisasa zaidi zinazoletwa na kiwanda.

Aidha amewaasa vijana kujiunga na chuo hicho na waondoe fikra kuwa kilimo ni cha jembe la mkono pekee kwani sasa kuna teknolojia za kisasa nyingi ambazo kijana anaweza kufanya kilimo katika maeneo mbalimbali kama wao walivyofanikiwa kufanya kazi katika viwanda hivyo wakione kilimo kama fursa tofauti na zamani.


Akizungumzia lengo la kuwatembelea wanafunzi hasa katika Kiwanda cha Sukari cha Bagamoyo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko Bi. Suzana Magobeko amesema ni kujionea namna wanafunzi wahitimu na wanaofanya mafunzo kwa vitendo ili kuboresha mitaala yake zaidi.

Amesema pamoja na kupokea pongezi kutoka kwa kiwandani lakini SUA inaona fahari kushikirikiana na Sekta binafsi kama Makampuni ya Bakhresa ambayo yamekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na mazao ya kilimo lakini pia kwa kujenga muhusiano ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu, SUA kuleta wanafunzi wajifunze kwa vitendo na kiwanda kinapokuwa na nafasi za ajira basi wanafunzi wa SUA wapewe nafasi.

   

KATIKA VIDEO 

Post a Comment

0 Comments