SUAMEDIA

Wakulima watakiwa kupima udongo kwa Uzalishaji wenye tija katika kilimo

 

Na: Siwema Malibiche, Tatyana Celestine

Wananchi wametakiwa kuzingatia upimaji wa udongo katika mashamba yao kabla ya kuanza kupanda mazao ili kutambua ubora wa udongo, kilimo anachotakiwa kulima pamoja mbolea ya kutumia ili kufanya  uzalishaji wenye tija  kwa maslahi binafsi na Taifa kwa ujumla.

                    

Mkuu wa Maabara kutoka  Idara ya  Sayansi za Udongo na Jiolojia  Chuo Kikuu cha Sokoine  cha  Kilimo   (SUA) Bw.  Amour Mohamed amebainisha kuwa upimaji wa udongo unasaidia kutambua ubora na afya ya udongo ambapo inampa uwezo mkulima kutumia maabara hiyo kutoa majibu ya maeneo sahihi kulingana  na mazao husika.

                              

Aidha amesema kuwa kupima udongo kuna faida ya kumfanya mkulima kutambua Tindikali, Naitrojeni, Fosforasi, Potashiam, Chumvi (EC) pamoja na aina ya udongo vitu ambavyo vinamsaidia kufanya uchaguzi wa mbolea atakazotumia shambani na mazao gani anaweza kulima katika eneo hilo.

Mkuu  huyo Maabara amesema wakulima wengi wamekosa elimu ya upimaji udongo kabla ya kuanza kilimo na kujihusisha na kilimo cha mazoea ambacho hakina faida kwao hivyo ni wakati kwao sasa kutambua  elimu hiyo ya afya ya udongo na mimea ni muhimu pasi kusubiri kupeleka sampuli zao katika maabara baada ya kuona madhara.

                                

Alipotakiwa kusema ni kitu gani kingine wanapima mbali na udongo amesema kuwa kupitia Idara hiyo wanapima Mazao na Samaki ili kutambua ubora wake kwa mlaji pamoja na kuangalia kiwango cha madini Tembo (Heavy Metal) ambayo yanapatikana kwenye udongo au madawa yatumikayo shambani kwani yakizidi hupelekea magonjwa kama kansa kwa mlaji.

Katika hatua nyingine Bw. Mohamed amesema SUA imekuwa na kawaida ya kuwatembelea wakulima walipo pindi panapokuwa na mradi ambao unalipa gharama zote lakini kwa sasa wanatakiwa kufika kufanya vipimo na kupata ushauri wa kubadili mazao ili kuepuka hasara zinazopatikana kwa kufanya kilimo cha mazoea .






 

 

 

 

 

 

 

 

Post a Comment

0 Comments