Na loyce Sikira, Shabani Ramadhani,
Wananchi hasa wakulima nchini wametakiwa
kujua elimu ya ulimaji wa zao la kahawa, jinsi ya kulihudumia zao hilo na namna
ya upatikanaji wa mbegu bora ambapo kwa kuzingatia hayo upo uwezekano wa kulima
zao hilo kwenye eneo lolote.
Amebainisha
hayo Bw. Godwin Rwezaula Afisa Kilimo Mwandamizi kutoka Ndaki ya Kilimo,
Idara ya Mimea Vipando na Mazao ya Bustani katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA), wakati akizungumza na SUA Media
kuhusiana na elimu ya zao la kahawa lakini pia uzalishaji wake kitaalamu ili kujiongezea
kipato chao na cha Taifa kwa ujumla.
Amesema kuna aina kuu mbili za kahawa zinazozalisha SUA ambazo ni Robusta na Arabika na kati ya hizo kuna aina nyingine nyingi ambazo zimetoka katika Taasisi ya Utafiti Arusha na wao wanazifanyia utafiti ili kuzijaribu na kuona kiikolojia kama zinaweza kulimwa vizuri Mkoani Morogoro
Aidha Bw. Rwezaula amesema kwa kawaida kahawa hulimwa
na kustawi vizuri sehemu za ukanda wa juu kama Kilimanjaro, Kigoma, Tabora,
Mbeya pamoja na Mbinga na kwa Mkoa wa Morogoro zao hilo linaweza kulimwa vizuri
katika maeneo ya ukanda wa juu kama vile Kinole, Matombo na Mkuyuni hivyo wao
kama SUA kupitia tafiti wanazofanya wamegundua kuwa hata ukanda wa chini zao
hilo linaweza kufanya vizuri endapo mkulima atazingatia namna bora ya ulimaji.
“Zipo aina bora za mbegu ya kahawa
ambazo zina uwezo wa kustahimili katika maeneo ya ukanda wa chini hasa kwa Mkoa
wa Morogoro hivyo mkulima akitambua aina hizo bora za mbegu ya kahawa na
kufuata hatua kwa hatua namna bora ya uzalishaji wa zao hilo anaweza akazalisha
kwa tija”, amesema Bw. Rwezaula.
Bw. Rwezaula ameongeza kuwa kati
ya mambo ya msingi kwa mkulima anayeanza uzalishaji wa zao la kahawa ni lazima
kuangalia Ikolojia aliyopo endapo inafaa kwa ajili ya zao hilo na baadaye kujua
chanzo cha vipando ambavyo anahitaji kwa ajili ya kahawa hivyo kwa sasa
wanashauri wapande kahawa bora kwa njia ya vikonyo ambapo kuna vitalu maalumu
vikiwemo vya Serikali.
0 Comments