Na:
Winfrida Nicolaus
Idadi ya Wahitimu katika Mahafali ya katikati ya mwaka kwa masomo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) imeongezeka kutoka Wahitimu 274 kwa mwaka 2023 hadi 777 kwa mwaka 2024 ikiwa ni ongezeko la asilimua 183.6 ambapo kati ya hao watunukiwa wanawake ni 284 sawa na asilimia 36.5 ya wahitimu wote.
Amebainisha
hayo Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda wakati akitaja takwimu
za Wahitimu katika Mahafali hayo yaliyofanyika Mei 23, 2024 katika viwanja vya
Michezo vya Kampasi Kuu ya Edward Moringe ambayo yamehudhuriwa na viongozi
mbalimbali akiwemo Mkuu wa Chuo hicho Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba ambapo amesema
wahitimu hao wametokana na programu 72 za masomo zinazofundishwa chuoni hapo.
Prof. Chibunda amesema wanastahili kujipongeza kwa mafanikio ambayo wameendelea kuyapata kila mwaka ya kuongeza idadi ya nguvu kazi yenye Taaluma stahiki, ujuzi na weledi ambayo ni chachu ya kuongeza maendeleo katika nchi na mafanikio hayo yanatokana na ufanyaji kazi mzuri wa viongozi, wahadhiri na wafanyakazi wote wa Chuo hicho ambao wamewezesha kupiga hatua zaidi mwaka hadi mwaka.
Aidha,
Prof. Chibunda amewaasa wahitimu kuendelea kuwa na bidii, uaminifu na moyo wa kujituma
waliokuwa nao wakati wa masomo kwenye sehemu zao za kazi ili na huko waweze
kufanikiwa vilevile kuwa mabalozi wazuri wa Chuo chao kwa kutumia maarifa na
ujuzi walioupata chuoni hapo kutatua changamoto katika jamii kwa maendeleo yao
binafsi na Taifa kwa ujumla.
“Mahafali
ni tukio la kipekee sana popote pale duniani kwa wahitimu, tukio hili ni muda
mahsusi wa kusheherekea, ni muda pekee wa kutathmini na kutafakari mafanikio ya
miaka kadhaa katika kufikia malengo
waliojiwekea, juhudi walizozionesha katika masomo yao, uaminifu na moyo wa kusoma na kufanya kazi waweze
kuonesha katika mahala pao pa kazi”, amesema Prof. Chibunda.
Ameongeza
kuwa Chuo kimeendelea kutekeleza malengo na majukumu yake kupitia katika Ndaki
zake zote, Shule Kuu ya Elimu, Kurugenzi na Taasisi zake tangu Mahafali ya 42 Novemba
2023 ikiwemo utekelezaji wa shughuli za mafunzo ambazo zimeendelea kufanyika
chuoni hapo kama ilivyopangwa katika Kampasi zote tatu kwa maana ya Edward
Moringe, Solomon Mahlangu pamoja na Kampasi ya Katavi.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Jaji
Mstaafu Mohamed Chande Othman amesema wahitimu hao wanapohitimu masomo yao hawamalizi
tu kama wahitimu bali viongozi watarajiwa, wavumbuzi na vijana walio tayari
kuchangia katika maendeleo ya nchi hususani katika Sekta ya Kilimo na fani
nyinginezo.
“Mzitumie
elimu na mafunzo mliyopata kuwa wabunifu na kufanya uvumbuzi wa Maendeleo
endelevu kwa ustawi wa jamii niwakumbushe tu dhamira ya Chuo chetu ni kukuza
maarifa, uvumbuzi na kukuza maendeleo endelevu ya ustawi wa jamii hivyo mkawe
mabalozi wazuri”, amesema Jaji Mohamed Chande.
0 Comments