Na:Tatyana
Celestine
Katika kuelekea
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Mei Mosi Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za
Elimu ya Juu Tanzania (THTU) Tawi la SUA wamefanya Kikao cha Mwaka pamoja na kutoa
mafunzo mbalimbali kwa wanachama wake lengo ikiwa ni kuwakumbusha masuala
muhimu ya kuzingatia wawapo kazini hata mara baada ya kustaafu.
Katika kikao hicho wanachama wamepata kujifunza mambo yahusuyo Afya, jinsi ya matumizi na kuweka akiba, Mafao na kikokotoo lakini pia namna bora ya kufuatilia haki zao kwa kutambua sheria za msingi za chama hicho pamoja na kufahamishwa namna watakavyoweza kupata msaada wakipata changamoto wawapo kazini.
Akizungumza
na SUAMEDIA wakati wa kikao hicho Dkt. Erhard Kapilima kutoka Kurugenzi ya Huduma
za Afya Hospitali ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA ambaye pia ni mtoa mada
kuhusu Afya amewaasa wafanyakazi wote kujua namna bora ya kuishi, kuzingatia kufanya vipimo mara kwa mara pamoja
na kupata matibabu stahiki kwani asilimia kubwa ya wafanyakazi kwasasa
wanafariki kutokana na magonjwa yasiyoambukiza kama vile Shinikizo la damu (Presha),
Kansa, Msongo wa Mawazo, Kisukari tofauti na miaka ya zamani.
Dr. Kapilima
ameongeza kuwa mtindo wa maisha wa sasa umesababisha watu wengi kuona hayo ndio
maisha bora lakini kwa upande wa afya ni tatizo kubwa kwani wamekuwa
hawazingatii vyakula sahihi, wanabobea katika matumizi ya pombe, uvutaji
sigara, na Shisha ambapo vyote hivyo sio salama kwa afya ya mwanadamu hivyo wanatakiwa kujenga tabia ya
kufanya mazoezi, kula vyakula vya asili na kuachana matumizi ya vilevi ili
kuepuka magonjwa yasiyo ya lazima,
Kwa upande
wake Afisa Sheria wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania
(THTU) Taifa Wakili Mohamed Kusekwa amesema kuwa wafanyakazi wengi hawana
taarifa sahihi zinazohusu haki zao wawapo kazini wengine kufikia kukubali
makosa wanapokosea kwa kuambiwa watasamehewa ili hali katika sheria za kazi
hakuna msamaha bali watapewa adhabu
kulingana na kosa alilotenda hata kama akikubali kosa husika.
Wakili huyo
amebainisha kwamba kila mfanyakazi anatakiwa kujua sheria na taratibu za Chama
chake cha wafanyakazi alichojiunga lakini pia kutofanya maamuzi ya kisheria
bila kupata ushauri unaofaa kutoka kwa wanasheria wao nao waweze kuwasaidia
pindi waingiapo kwenye migogoro na waajiri wao kufanya hivyo itawasaidia kupata
haki bila kikwazo.
Naye Dkt.
Prisila Mkenda Mhadhiri SUA kutoka Idara ya Sayansi ya Viumbe Hai ambaye pia ni
mwanachama wa THTU alipotakiwa kuzungumzia faida ya kikao hicho kupitia chama chao amesema
utaratibu wa Chama chao kutoa elimu ni
suala mtambuka kwani inamfanya mfanyakazi kutambua alikotoka alipo na anapoelekea
katika nyanja zote ikiwemo Afya, Stahiki za uzeeni, sheria, namna ya kuweka
akiba na matumizi ya fedha wawapo kazini.
Ameongeza kuwa kwa upande wa Afya kwa kuwa wao
wamekuwa na maisha yasiyo na mazoezi ya kuutosha mwili kwa kwenda ofisini kwa
gari, wanakula na kunywa wawapo ofisini na baadae kurudi nyumbani kwa kutumia
usafiri uleule kwa tathmini hiyo ni dhahiri hawana mazoezi ya kuutosha mwili
hivyo ushauri walioupata ni muhimu kwa kila mmoja wao kuuzingatia ili wawe na
afya bora sasa na hata baada ya kustaafu.
0 Comments