Na: Farida Mkongwe
Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
wamejengewa uwezo wa kutambua masuala ya usawa na uwiano wa kijinsia katika
Taasisi za Elimu ya Juu ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa kuzingatia fursa
sawa kwa makundi ya kijinsia yaliyopo chuoni hapo.
Hayo yamebainishwa na Profesa Msaidizi John Jeckoniah kutoka Idara ya
Taaluma za Maendeleo na Mafunzo Mkakati Machi 19, 2024 wakati akizungumza na
SUA Media katika mafunzo ya kuwajengea uwezo Wanataaluma wa SUA kuhusu mbinu za
kuboresha ufundishaji kwa Wanataaluma hao.
Prof. Jeckoniah amesema Taasisi za Elimu ya Juu zimekuwa
zikipata changamoto myingi zinazohusiana na kutokuwepo kwa usawa na uwiano wa
kijinsia na kwamba mafunzo hayo yatawajengea uwezo Wanataaluma kutambua kwa
ufasaha suala la usawa wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kutambua vitendo vya
ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ambavyo vimekuwa vikiwaathiri zaidi wanawake
katika mazingira tofauti.
“Kwanza kabisa kumekuwa na uelewa mdogo kwa wanataaluma kuhusu
masuala ya jinsia kwa upana wake, wakijengewa uwezo namna ya kutambua vitendo
hivi vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia itasaidia sana maana vitendo hivi
wakati mwingine vinatokana na mila, desturi na tamaduni ambazo tumekuwa nazo
katika malezi na makuzi yetu”, amesema Prof. Jeckoniah.
Amesema kuna ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia ambao pia
unajitokeza kwenye baadhi ya machapisho na vitabu vinavyotumika kufundishia
lakini hauonekani kwa urahisi na kutolea mfano machapisho au vitabu
vinavyotumia picha ya jinsia ya kiume kuonesha mtu ambaye ni mahiri katika kazi
zake au mtaalamu wa jambo Fulani na hivyo kujenga dhana potofu kuwa labda
wanawake hawawezi kufanya kazi zao kwa weledi kama wanaume.
“Hata inapoandaliwa mitaala sisi wataalamu wa jinsia tunapenda
kushirikishwa ili tuweze kuangalia kama mapungufu katika ufundishaji au kama
kuna upotofu kuhusu dhana zisizo sahihi ambazo zipo nyingi lakini mara nyingi
kwa sababu watu wamelelewa katika misingi hiyo hawaoni makosa hayo kwa hiyo
kuna dhana potofu na tusipopata namna ya kuzitatua zinaweza kuendelea”, amesema
Prof. Jeckoniah.
0 Comments