Na: Farida Mkongwe
Baadhi ya Wahadhiri Waandamizi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) wanaopata mafunzo ya kujengewa uwezo wa namna ya kuboresha
ufundishaji na usimamizi wa Shahada za Awali, Shahada za Uzamili na Uzamivu
wameipongeza Menejimenti ya Chuo hicho pamoja na waandaaji wengine kwa kuandaa
mafunzo hayo ambayo yatawaletea ufanisi katika utendaji wa kazi zao.
Wakizungumza na SUA Media Prof. Justin Kalisti Urassa kutoka
Idara ya Sera, Mipango na Usimamizi, Dkt. Khalfan Hamidu kutoka Idara ya
Misingi ya Utawala na Uongozi Elimu katika Shule Kuu ya Elimu, na Mkufunzi
Msaidizi Faines Msigwa kutoka Idara ya Infomatikia na Teknolojia wamesema
mafunzo hayo yamekuwa wakati muafaka kutokana na mabadiliko ya teknolojia
yanayotokea duniani kote kwa sasa.
“Kwa tunavyofahamu katika maisha kujifunza ni kitu endelevu na
unapojifunza unapata kitu kipya kinachoenda kuboresha utendaji wako, ukizingatia
SUA ni Chuo kinachopendwa na wanafunzi wengi hivyo mafunzo haya yatatuwezesha
kwenda kuwajenga wanafunzi wetu waweze kuwa na ubora zaidi na hivyo
wahitimu kuweza kukubalika ndani na nje ya nchi”, amesema Prof. Urassa.
“Kwa upande wangu nimeona manufaa makubwa kwa sababu kimsingi
mafunzo haya yamejikita katika suala zima la ubora katika huduma ambazo
tunazitoa kwa wanafunzi pamoja na huduma za kijamii kwa wanajumuiya wa SUA, na
yatatusaidia kwa sababu wanatunoa vizuri kiakili, kiujuzi na kiufahamu,
tunawapongeza kwa sababu wanatufundisha misingi ya kuzingatia kwenye masuala ya
utoaji wa elimu fundishi, elimu ongozi lakini pia katika kufanya vitu kwa
ufanisi na kuzingatia ubora”, amesema Dkt. Hamidu
Kwa upande wake Mkufunzi Msaidizi Faines Msigwa amesema
anaendelea kujifunza kutoka kwa wataalamu mbalimbali na wawezeshaji mahiri
waliopo kwenye mafunzo hayo.
“Mpaka sasa nimejua sheria ambazo mwananfunzi anatakiwa
azifuate wakati wa mitihani na je mwananfunzi akikutana na kosa fulani ni nini
kinatakiwa kifanyike kwa huyo mwananfunzi, natumai nitaendelea kujifunza na
nikitoka hapa nitakuwa nimejua mambo mengi”, amesema Mkufunzi huyo Msaidizi.
0 Comments