SUAMEDIA

Morogoro kuanza kulima zao la Tumbaku ili kunufaika na uwepo wa Viwanda vya Usindikaji Mkoani humo.

 Na: Calvin Gwabara – Tabora.

Mkoa wa Morogoro umejiandaa kunufaika na uwepo wa viwanda vya usindikaji wa Tumbaku kwa kuanzisha kilimo cha zao la Tumbaku kwa kuanzia na wilaya ya Gairo na katika kufanikisha adhma hiyo, ushirikishwaji wa wataalamu wa zao hilo imekuwa sehemu ya mkakati huo muhimu kwa mkoa.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania (TORITA), Dkt. Jacob Bulenga Lisuma wakati akiongea na Waandishi wa habari ofisini kwake.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania (TORITA), Dkt. Jacob Bulenga Lisuma wakati akizungumza na SUAMEDIA kuhusu mipango na fursa zinazoibuliwa na Taasisi hiyo katika kukuza uzalishaji wa zao la Tumbaku nchini. Akitanabaisha zaidi juu ya mkakati wa kuanzisha kilimo cha Tumbaku kwa kushirikiana na Serikali ya mkoa na wilaya, Mkurugenzi huyo alisema;

“Hivi karibuni mnamo mwezi wa nane nilialikwa kwenye kikao cha baraza la madiwani Wilayani Gairo kushiriki mjadala wenye lengo la kutafuta jinsi bora ya kulima Tumbaku na kulifanya zao hilo kuwa la msingi wa kiuchumi ili kunufaika na uwepo wa Viwanda vya kusindika zao hilo mkoani Morogoro. Hili lilizingatia kwamba wananchi wa Morogoro hawajaweza kutumia vema fursa wanastahili kutokana na uwepo wa viwanda hivyo kwa sababu hawalimi zao husika” alieleza Dkt. Jacob.

Aliongeza “Kwahiyo tulitembelea wilayani Gairo na kuwapa ushauri ya kwamba wao waweze kuzalisha aina ya Tumbaku ambayo inakaushwa kwa Jua kwa sababu Wilaya ya Gairo haina miti ambayo ni uoto wa asili hivyo itakuwa ni kinyume cha utunzaji wa mazingira iwapo watalima aina ya tumbaku ya kukaushwa kwa moshi. Alionyesha kufurahishwa na muitikio mkubwa wa wananchi na uongozi wa wilaya kwa ujumla na namna walivyojipanga kuhakikisha kwamba lengo lao linatimia. Gairo wameiandikia bodi ya Tumbaku Tanzania ili wawekewe utaratibu kama wakulima wengine na waanze mara moja uzalishaji wa tumbaku aina ya Balley inayokaushwa kwa jua”. 


Alisisitiza utayari wa Taasisi ya TORITA katika kuwasaidia wakulima wa Gairo ili walime kitaalamu na kuleta ufanisi kama ilivyo katika mikoa mingine ya Tabora, Katavi na Kigoma.

Aidha, amesema kwakuwa  mahitaji ya watu wanataka kulima zao hilo ni makubwa Dkt. Jacob  ametumia mwanya huo kupitia SUAMEDIA kuwakumbusha wakulima kuacha Kilimo cha mazoea na badala yake wajisajili bodi ya tumbaku na kupata namba za utambuzi ili ziwasaidie kupata pembejeo na kupangiwa chama cha msingi husika ambacho watauzia tumbaku yao.

Mkurugenzi huyo amesema, pamoja na Zao la Tumbaku kuonekana kuwa ni la Mkoa wa Tabora kwa sasa TORITA imesaidia kufanya tafiti za maeneo mbalimbali yanayofaa kulimwa zao hilo nchi nzima na mpaka sasa Tumbaku inalimwa katika Mikoa na wilaya mbalimbali zikiwemo wilaya ya Kasulu (Kigoma), Kahama, Biharamulo, Chunya (Mbeya), Mpanda (Katavi) na maeneo mbalimbali ya mikoa ya Mara, Iringa na Songea.

Ametanabaisha kwamba, pamoja na mikoa hiyo kuongea uzalishaji wa Tumbaku, Mkoa wa Mara una maeneo mengi yanayolimwa na yanayoandaliwa kuanza kilimo cha tumbaku hivyo umeombewa kwenye Bodi ya Tumbaku kuwa Mkoa wa Kilimo hicho.

Ramani ya Tanzania ikionesha ulipo Mkoa wa Morogoro.


Post a Comment

0 Comments