Na, Winfrida Nicolaus
Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Mradi wa Mkulima GPT chini ya
ufadhili wa ‘BILL na MELINDA GATES Foundation’ imetoa mafunzo kwa wakulima
wadogowadogo wapatao 20 mkoani Morogoro
kuhusiana na Mfumo wa Akili Bandia unaotumia lugha ya kiswahili utakaomsaidia mkulima
kuweza kupata ushauri kuhusiana na kilimo cha Mahindi kwa wakati husika lakini
pia kutatua tatizo kwenye shamba lake bila uwepo wa Afisa Ugani.
Kiongozi wa Mradi huo na Mhadhiri Msaidizi SUA kutoka Idara ya Infomatikia na Teknolojia ya Habari Bi.Theofrida Maginga akizungumza na wakulima na wadau wa kilimo |
Amebainisha
hayo Kiongozi wa Mradi huo na Mhadhiri Msaidizi SUA kutoka Idara ya Infomatikia
na Teknolojia ya Habari Bi.Theofrida Maginga wakati akizungumza na SUAMEDIA
kwenye warsha iliyofanyika katika Hoteli ya Morena iliyoko Msamvu mjini Morogoro
ambapo amesema Mkulima GPT ni ‘Chatbot’ inayowasaidia wakulima kupata
taarifa ya namna ya kuandaa mashamba vilevile kusimamia mashamba ya kilimo cha
mahindi kwa kutumia Akili Bandia ( Artificial intelligence).
Amesema lengo
la kutumia Akili Bandia ni kwasababu ya ukuaji wa teknolojia hivyo wao kama watafiti
kutoka SUA wanaangalia namna mbalimbali ambazo wanaweza wakatumia teknolojia
kuwasaidia wakulima katika kufanya shughuli zao za kila siku japokuwa
teknolojia inaweza kutumika si kwenye kilimo pekee bali hata kwenye maswala
mbalimbali ya kijamii lakini kwa kuanza Mkulima GPT imelenga kuanza na kilimo
cha Mahindi na hapo baadae wataangalia na mazao mengine,
Aidha Theofrida
Maginga amesema wameleta Teknolojia hiyo kwa Wakulima ili wawe sehemu ya ukuaji
wa teknolojia hiyo ndio maana wamefanya warsha ya kuwafindisha Wakulima hao namna ya kutumia Mkulima GPT ili
waweze kuanza kilimo cha kisasa ambacho kinafanyika si kwa kutumia Matrekta
pekee lakini pia hata kutumia Akili bandia katika kufanya shughuli za kila siku
kwa Mkoa wa Morogoro lakini pia na Tanzania kwa ujumla.
“Nafahamu
kuwa sisi sote tunafahamu kuwa teknolojia ni changamoto kwa maeneo ambayo
hayafikiki au maeneo ya vijijini sana lakini teknolojia inakuwa na lazima tujifunze
kuwa nayo na lazima tutengeneze matokeo ambayo yanaweza kuwasaidia wakulima kutumia
hii hivyo basi mkulima anaweza akawa na namba ya simu ya ‘WhatsApp’ tu
na akauliza swali kuhusiana na kilimo cha mahindi kwa kutuma ujumbe maandishi
au sauti na moja kwa moja akapata majibu ya maelezo kutokana na swali
alilouliza”, alisema Bi Theofrida Maginga
Akifungua
mafunzo hayo Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
Prof. Samwel Kabote amesema hatua uliyofikiwa katika matumizi ya Akili Bandia
ni kubwa na itawasidia wakulima kupata taarifa kwa wakati.
Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Samwel Kabote akifungua mafunzo |
Amesema Chuo
Kikuu cha Sokoine kitaendelea kuhakikisha kinasaidia watafiti wachanga katika
kuleta tafiti, ubunifu na teknolojia rafiki kwa wakulima ili ziwe na tija.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa
Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu (SUA) Prof. Esron Karimuribo amesema teknolojia
hiyo ni zaidi ya utafiti ni muendelezo wa kuboresha shughuli za Ugani kwa
wakulima nchini ambapo Akili Bandia inatumika kusaidia katika kutoa ushauri wa papo
kwa papo na kitu kizuri zaidi Utafiti huo umetumia lugha ya watanzania wengi
ambayo ni kiswahili lakini pia imetumia ule mfumo wa ‘WhatsApp’ ambao
watu wengi wameuzoea.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu (SUA) Prof. Esron Karimuribo akizungumza katika mafunzo hayo |
Amesema ili
kuboresha matokeo makubwa ya kazi hii taasisi na vyombo husika na maswala yote
ya Tehama pamoja na habari ikiwemo TCRA, EGA pamoja na Wizara ya Mawasiliano inabidi
waione hii kama huduma muhimu kwa Taifa ikiwezekana yawekwe mazingira rafiki
kuanzia bei za vifurushi na upatikanaji wa simu za ‘WhatsApp’ kwa njia
rahisi ili wakulima wengi ambao wanahitaji huduma hiyo kuweza kuwa na nyenzo
hizo pamoja na uwezo wa kidedha kuweza kupata huduma hiyo kwa haraka zaidi.
“Kupitia teknolojia
hii kuna wakati hata hautahitaji Afisa Ugani katika eneo husika bali Afisa
Ugani kiganjani hivyo nitoe rai kwa wakulima
kuanza mara moja kutumia teknolojia hiyo ambapo tupo sasa kwenye msimu wa
kilimo hivyo natamani kuona mwaka huu huu teknolojia hiyo imeanza kutumika
katika kuboresha mazao na tija ya uzalishaji hasa kwa zao la Mahindi”, alisema
Prof. Esron Karimuribo
Naye Bi.
Nia Sifanani ambaye ni Mkulima amesema kuwa mfumo wa Mkulima GPT ni mfumo mzuri
ambao utaenda kuwasaidia wao kama wakulima kutatua changamoto mbalimbali ambazo
zinawakabili shambani na hata kwenye mazingira mengine hususani katika ufuatiliaji
wa mazao hata hivyo ameiomba Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa kilimo
nchini kuweza kuwasaidia katika upatikanaji wa mtandao kiurahisi hasa kwa wakulima
waliopo vijijini.
Habari Picha 👇
0 Comments