SUAMEDIA

SUA yatekeleza adhma ya Mhe. Rais Samia kwa uchangiaji wa damu wa hiari

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Mipango, Fedha na Utawala Prof.  Amandus Muhairwa ameipongeza Serikali ya wanafunzi ya  Chuo hicho kwa kufanya Kampeni ya kuchangia damu, kwa lengo la kutekeleza adhima ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.  Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuokoa maisha ya wenye uhitaji wa damu nchini.


Akifungua Kampeni ya Uchangiaji Damu ambayo imefanyika katika Kampasi ya Edward Moringe, Morogoro Prof. Muhairwa amewataka wanafunzi kuitikia wito wa viongozi wao wa Serikali ya wananfunzi na kuona umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari kwani ni chachu ya kuokoa maisha ya wahitaji wa damu katika nchi yao hivyo waendelee kutekeleza kampeni hiyo muhimu ili damu ipatikane na ikawe msaada kwa Taifa.

"Niwapongeze sana kwa wazo hili, ni jambo ambalo linaenda kugusa maisha yetu ya kila siku, na Mungu anatuhimiza kuwa watoaji zaidi, sisi (Menejimenti ya SUA) tuko pamoja nanyi na tutaendelea kuwapa ushirikiano mnaohitaji ili malengo yenu yatimie". Alisema Prof. Mhairwa.

Nae Rais wa Serikali ya Wanafunzi SUASO Mhe. Abdul-Fatah Ibrahim akizungumza wakati wa uzinduzi huo amesema kuzindua kampeni hiyo ikiwa ni katika kuenzi mawazo wa Rais wa TAHLISO ambayo inalenga wanafunzi wa elimu ya juu kwa vyuo vyote nchini kuwa na utaratibu wa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya binadamu wakiwepo wanaopata majeruhi, wanawake wajawazito na watoto.

Aidha ameongeza kuwa Serikali ya wanafunzi imekusudia kuwa na zoezi hilo mara kwa mara kutokana na uhitaji wa damu  uliopo katika vituo mbalimbali vya kutolewa huduma za afya nchini.
















Post a Comment

0 Comments