Na: Calvin Gwabara – Morogoro.
Jopo la Watafiti katika Mradi wa
Utafiti wa Mazingira ya Chakula katika Miji na kuboresha lishe ya Walaji (FETE)
wamekutana kuzindua mradi na kupanga mikakati ambayo itasaidia kuimarisha lishe
ya jamii na kupunguza utapiamlo kwa nchi nne za Afrika zinazoshiriki utafiti
huo.
Mtafiti Mkuu wa mradi wa utafiti wa (FETE) kwa upande wa Tanzania Prof. Joyce Kinabo akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo. |
Hayo
yamebainishwa na Mtafiti Mkuu wa mradi huo kwa upande wa Tanzania Prof. Joyce
Kinabo ambaye ni Profesa wa lishe wakati akitoa utambulisho wa Mradi huo kwa
jopo hilo linalohusisha watafiti kutoka Tanzania, Ghana, Afrika ya Kusini,Malaysia
na Ujerumani kwa ufadhili wa Shirikisho la Shirika la Kilimo na Chakula la
Ujerumani (BLE).
“Wengi mtakubaliana na mimi kuwa tuna
matatizo makubwa ya utapiamlo wa chini na utapiamlo wa juu kwa maana kwamba
uzito ulikithiri na unene unazidi kuwa changamoto kwa watu wengi hapa Tanzania changamoto
ambayo inachangiwa na mazingira hafifu na mabaya ya chakula”, alieleza Prof.
Kinabo.
“Vyakula vingi ambavyo tunaviona kwenye maduka
yetu na supermarket vingi ni vile vya
kusindikwa na vingi vinakuwa na sukari nyingi,Mafuta mengi na hivyo kusababisha
mlaji kuchukua wanga au sukari zaidi ya mahitaji ya mwili wake na hii humfanya mtu aongezeke uzito kwa kasi na hivyo
kupelekea kupata magonjwa yasiyo ya kuambukizwa mfano Kisukari, Shinikizo la
damu na magonjwa ya moyo”, aliongeza Prof. Kinabo.
Hivyo amesema utafiti huo
unalenga kuboresha mazingira ya masoko na maeneo yote yanayouza chakula ili
waweze kuuza vyakula ambavyo vitampatia mlaji lishe bora kama vile matunda, mbogamboga
na jamii ya mikunde na sio vyakula ambavyo vinaenda kumuongezea matatizo hasa vilivyosindikwa sana na kuongezea sukari
nyingi na mafuta mengi.
Prof. Kinabo amesema kuwa utafiti
huo utatoa somo na suluhisho la nini kifanyike kwa upande wa wadau, Sera, na wauzaji
wa vyakula ili kwa pamoja waweze kuipa jamii chakula kitakachosaidia kuimarisha
lishe za afya za watu.
Amesema Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo kinanufaika hasa kupitia wafanyakazi wake kupata ufadhili wa masomo
katika shahada za Uzamivu lakini pia wanataaluma watafiti kwenye mradi huo
kupata nafasi ya kuchangamana na wenzao kutoka nchi zingine na kuongeza uzoefu
na mashirikiano katika maeneo ya utafiti.
Akizungumzia kilichowasukuma kutekeleza
mradi huo wa utafiti Mratibu wa Mradi huo kwa nchi zote nne Dkt. Daniella
Waible kutoka Taasisi ya Uchambuzi wa Masoko ya Thenen ya nchini Ujerumani
amesema ni tatizo kubwa la utapiamlo,Ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza
na hasa zinazoathiri ukuaji wa uchumi ambapo tabia za kilishe zinapitia
mabadiliko makubwa.
Mratibu wa Mradi huo kwa nchi zote nne Dkt. Daniella Waible kutoka Taasisi ya Uchambuzi wa Masoko ya Thenen ya nchini Ujerumani akitoa neno wakati wa uzinduzi wa mradi. |
“Lengo kubwa ni kuanzisha
ushirikishaji wa tatizo na fursa, kuleta suluhisho la kutengeneza mazingira
bora ya chakula, kutoa mfano wa marejeo, kutoa modeli ya marejeleo ya jinsi
mbinu zilizoanzishwa na matokeo yaliyopatikana yanavyoweza kutumika kwa upana zaidi
katika Kusini mwa dunia kwa kuwalenga watu wa hali ya chini mijini”, alifafanua
Dkt. Daniella.
Mratibu huyo wa mradi huo wa
utafiti amesema andiko la mradi kwa wafadhili liliwasilishwa toka mwaka 2019 na
kupitia michakato mbalimbali na hatimae mwezi wa 12 mwaka 2022 ndio
likakubaliwa na hivyo akatumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau wote walioshiriki
kwa uvumilivu na michango yao ya mawazo katika kufanikisha mradi huo muhimu kwa
maendeleo ya nchi zote.
Akifungua mkutano huo Mkurugenzi
wa Kurugenzi ya Shahada za Juu, Utafiti na Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri
wa Kitaalamu (DRPTC) Prof. Esron Karimuribo kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda amepongeza uchaguzi wa mada
ya Utafiti huo na kwamba umekuja wakati muafaka ambapo kumekuwa na changamoto
kubwa ya ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukizwa yanayohusishwa na lishe
duni.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Shahada za Juu, Utafiti na Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu (DRPTC) Prof. Esron Karimuribo akifungua Mkutano wa uzinduzi wa mradi huo wa FETE. |
“Tunashuhudia vifo vya watu wetu
vinavyotokana na wao kutokujua mambo ya msingi tu ambayo yanahusiana na lishe
hivyo sisi kama nchi lakini pia katika ukanda huu tunapongeza mada ya utafiti
huu mliyochangua kwakuwa inakwenda kujibu changamoto hizo ambazo zinaathiri
afya za jamii zetu”, alifafanua Prof. Karimuribo.
Hata hivyo kwa niaba ya Uongozi
wa SUA, Prof. Karimuribo amewahakikishia watafiti hao ushirikiano wa kutosha
katika kufanikisha utekelezaji wa mradi na kuwaeleza kuwa wamechagua mahali
sahihi kutokana na Chuo hicho kuongoza kwa miaka mitano mfululizo kwenye
masuala ya Utafiti na machapisho nchini Tanzania hivyo wanafanya kazi na
taasisi bora nchini.
Jopo la watafiti wa Mradi huo wa
FETE linajumuisha watafiti na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo nchini Tanzania,Taasisi ya uchambuzi wa Masoko ya Thunen ya Ujerumani,
Taasisi ya Utafiti wa masuala ya Sera za
Sayansi na Tenolojia (STEPRI) ya nchini Ghana, Chuo Kikuu cha Nottingham
cha Malaysia na Chuo Kikuu cha KwaZulu – Natal cha Afrika ya Kusini.
Picha ya pamoja ya jopo la watafiti kutoka nchi tano zinazotekeelza mradi huo wa utafiti |
Mtafiti Mkuu wa Mradi huo kwa upande wa Tanzania Prof. Joyce Kinabo (Kushoto) akipokea zawadi kutoka Ujerumani kwa niaba ya wanajopo hilo zilizokabidhiwa na Dkt. Johanna Schott. |
0 Comments