Na: Calvin Gwabara – Mbarali.
Matokeo ya Utafiti wa
miaka miwili kuangalia Mtiririko wa maji na afya ya Mto Mbarali Mkoani Mbeya
yameonesha kuwa Maji yanapungua na hii ni kutokana na ongezeko la watu na
mahitaji ya matumizi ya maji kuongezeka sambamba na uharibifu wa vyanzo vya
maji vya mto huo.
Mtafiti Mkuu wa Mradi wa EFLOWS Prof. Japhet Kashaigili akiwasiliasha matokeo ya utafiti huo mbele ya wadau kwenye warsha iliyofanyika Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya. |
Hayo yamebainishwa na
Prof. Japhet Kashaigili kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambaye
ni Mtafiti Mkuu wa Mradi huo wa miaka miwili wa Utafiti wa Usimamizi Endelevu wa Madakio ya Maji
Kupitia Tathmini ya Kuimarisha Mtiririko wa Maji kwa Mazingira na Utekelezaji
wake katika Kulinda Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi na Athari za
Shughuli za Kibinadamu Tanzania (EFLOWS) wakati akiwasilisha matokeo ya utafiti
huo kwa wadau wa maji wa mto Mbarali wilayani humo Mkoani Mbeya.
“Tulichokiona kwenye
utafiti ni kwamba wingi wa maji kwenye mto unaendelea kupungua, wahitaji wa
maji wanaongezeka lakini pia mabadiliko ya tabia nchi nayo yameathiri kwa kiasi
kikubwa mtawanyiko wa maji na mvua kwenye maeneo haya na hivyo kupelekea maji
kupungua mtoni na athari zake hasi zikionekana kwenye mifumo ikolojia ya mto
hasa wakati wa kiangazi. Tumeona uwepo wa matumizi makubwa ya maji bila vibali
kwa kutumia pampu, na uzalishaji mkubwa wa mchanga wakati wa mvua kutokana na
shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya vyanzo milimani na kwenye mashamba”
alisema Prof. Kashaigili.
Aliongeza” Shughuli za
kibinadamu zinazofanyika Mbarali kwa maana ya makazi, kilimo, ufugaji,
ufyatuaji wa matofali kwenye vyanzo vya maji na mtoni, kilimo cha vinyungu,
moto na shughuli zingine za kibinadamu zimechangia kwa kiasi kikubwa mtawanyiko
wa maji kwenye mto, lakini uchukuaji wa maji kwenye mto ndio umeonekana
kuongoza kwa athari hasi”.
Prof. Kashaigili
amesema changamoto hiyo ya matumizi makubwa ya maji imepelekea mto kukauka
kabisa maeneo ya chini wakati maeneo ya juu ya mto na katikati ukifika unakuta
maji mengi yanatiririka ambayo hayafiki mwisho yanaishia njiani kutokana na
watu kuyachepusha na kuyachota kwaajili ya shughuli zao mbalimbali hususani
kilimo ambacho hakizingatii matumizi sahihi ya maji hayo.
“Kwa maana hii ni
kwamba Mto Mbarali hauchangii chochote kwenye Mto Ruaha Mkuu hasa wakati wa
kiangazi kwenye maeneo ya uhifadhi na hii maana yake ikolojia ya mto na
uendelevu wake imeathirika na hivyo kushindwa kufikia malengo makubwa ya
Kidunia ya maendeleo endelevu na yale ya kitaifa ya kuifadhi na kuilinda
baonuai ya mto” alifafanua Mtafiti huyo Mkuu Prof. Kashaigili.
Mtafiti huyo aliyebobea kwenye tafiti za Masuala ya maji na Mazingira Duniani amesema pamoja na Utafiti kutoa matokeo hayo kwa wadau hao muhimu pia wameainisha njia na mikakati ya kufanya ambayo ikifanyika itasaidia kupunguza athari zilizojitokeza na kusaidia kurejesha afya ya mto na mtiririko wa maji kwenye Mto Mbarali na mingine nchini kwa kuwa changamoto zinafanana.
Amesema moja kati ya
mikakati hiyo ilikuwa kurejesha uoto wa asili kwenye vyanzo vyote vya maji
vilivyoathirika na kingo za mito, ambapo mradi kwa kuanzia umesaidia kuanzisha
vitalu vikubwa viwili vya miti rafiki wa maji kwenye wilaya ya Wanging’ombe
Mkoani Njombe na Mbarali Mkoani Mbeya kwa kutumia elimu asili na kufanikiwa
kupanda miti zaidi ya elfu 45 kwenye vyanzo na kingo za mito pamoja na
kuanzisha ufugaji wa nyuki kwa ajili ya kuongezea kipato cha jumuiya za watumia
maji wanaosimamia madakio pamoja na kuongezea uhifadhi.
Kwa upande wake
Mtaalamu wa Sayansi za maji na Viumbe wake kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
Bw. Sherald Mkama ambaye alikuwa anaangalia afya ya mto na usalama wa maji
kupitia mradi huo amesema matokeo yameonesha maji yanayotiririka kwenye mto huo
bado ni salama kwa kuwa baada ya kufanya utafiti wamekuta viumbe ambao hawawezi
kuishi kwenye maji ambayo sio salama.
Mtaalamu wa Sayansi za maji na Viumbe wake kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Bw. Sherald Mkama akizungumzia matokeo hayo mbee ya Waandishi wa habari nje ya mkutano huo. |
“Viumbe wadogo
wanaoishi majini pamoja na samaki wanauwezo mkubwa wa kutoa ishara ya ubora wa
maji katika eneo na ndio maana pamoja na watafiti wengine huchukua sampuli za
maji na kuzipima, lakini mbinu ya kuangalia viumbe ndio muhimu zaidi kwa kuwa
ndio wanakaa kwa muda mrefu kwenye eneo hilo kuliko kupima maji maana unaweza
kwenda kuchota maji ukakuta wakati huo ni bora kwa muda huo tu, ila viumbe
waishio kwenye maji hawapiti wapo muda wote” alifafanua Mkama.
Mtafiti huyo amezitaka
mamlaka zinazosimamia maji kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi mzuri hasa
kwenye maeneo wanayochota maji mengi kwenye skimu ya Umwagiliaji ya Igomelo
ambayo wanatumia viuatilifu na mwisho sehemu ya maji hayo yanarudi mtoni yakiwa
na viambata sumu kama hawatazingatia matumizi salama ya viuatilifu, mwisho yaweza
pelekea kuua viumbe walio mtoni na kuathiri pia jamii inayotegemea maji ya mto
huo kwa matumizi ya nyumbani.
Naye Mtafiti aliyekuwa
anaangalia mimea iotayo kandokando ya mito na vyanzo vya maji Dkt. Emmanuel
Mwainunu kutoka Taasisi ya utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) amesema mimea
hiyo ni muhimu kwa kuwa ndiyo inayosaidia kuwepo kwa uhai wa mto kwa kutunza
maji, kufyonza mbolea na kuyafanya yatiririke kidogokidogo badala ya kasi
pamoja na kuzuia mmomonyoko wa kingo za mito.
Mtafiti aliyekuwa anaangalia mimea iotayo kandokando ya mito na vyanzo vya maji Dkt. Emmanuel Mwainunu kutoka Taasisi ya utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) akizungumzia eneo la utafiti wake. |
“Tunapoangalia hali ya
Uoto kwenye mito na afya ya mto huwa tunatumia madaraja A mpaka F, hivyo
tunaposema hali ya ukanda fulani ni A maana yake hakuna uharibufu katika eneo
hilo, lakini ikiwa daraja B ina maana eneo limeanza kupata athari za awali
lakini hazijaanza kuleta madhara, na ikishuka kufikia daraja D ina maana athari
ni kubwa sana na ikifikia daraja F ina maana eneo hilo limeharibika sana,
athari ni kubwa sana na madhara yake ni makubwa sana ambapo si rahisi
kurekebishika katika hali ya kawaida. Tathmini yetu imeonesha kuwa yapo
mabadiliko kadhaa ambayo yametokana na shughuli za kilimo na ufugaji lakini
kimsingi uharibifu wake kwenye uoto wa kandokando za mto sio mkubwa sana na
kupelekea kupata daraja B, hata hivyo ni
lazima jitihada zifanyike kusitisha changamoto hii kuendelea” alieleza Dkt.
Immanuel.
Amesema kuwa wamekuta
mimea kama vile Msandali ambayo ni mimea yenye matumizi mengi kama utengenezaji
wa Manukato pamoja na mimea mingine rafiki wa maji lakini inawezekana kutoweka
kwa kuwa jamii zinafanya shughuli mbalimbali kandokando ya mto huo na
kuiathiri, hivyo jitihada za makusudi zichukuliwe na mamlaka za usimamizi wa
mito kunusuru mto kuachwa wazi.
Mradi huu wa Utafiti
unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na
Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kutekelezwa
katika Bonde la mto Rufiji ndani ya dakio la mto Mbarali kwa ushirikiano na
Bodi ya Maji ya mto Rufiji, jumuiya za watumia maji, Wakala wa Huduma za Misitu
(TFS), Wilaya ya Mbarali na Wanging`ombe na jamii, kwa ufadhili wa program ya
Mazingira ya Umoja wa Mataifa, UNEP, kupitia michango ya nchi kumi wanachama wa
Azimio la Nairobi ambapo kwa Tanzania ni kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais,
Mazingira, katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Kivitendo wa Magharibi mwa
Bahari ya Hindi chini ya uratibu wa Sekretarieti ya Azimio la Nairobi.
0 Comments