Na: Asifiwe Mbembela
Wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari
ya Dkt. Salmin Amour Juma iliyopo Chumbuni Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar
wametakiwa kuchangamkia fursa ya kusoma katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) ili kuweza kutimiza ndoto zao.
Wito huo umetolewa na Mhadhiri wa Lishe na Sayansi ya Mlaji Bi.
Zahra Majili wakati akiongea na wanafunzi hao kwenye ziara maalum iliyofanywa na
baadhi ya wafanyakazi wa SUA kwenye shule hiyo kwa ajili ya kuwaelezea programu
ambazo zinatolewa na Chuo hicho, tukio lililofanyika katika Uwanja wa nje wa
Shule hiyo Agosti 02, 2023.
Bi. Zahra Majili amewaeleza wanafunzi hao kuwa ili waweze
kutimiza ndoto zao, wanaweza kujiunga na Chuo cha SUA kwani kimekuwa
kikiwaandaa wanafunzi kwa njia ya vitendo ambavyo vinawaruhusu hata baada ya
kuhitimu kuweza kujiajiri pamoja na masomo ya nadharia.
“Wanangu niwaambie tu mko hapa lakini kesho mtakuwa kwenye mahitaji
ya kujiunga na elimu ya juu, sasa mkifika hapo naomba mchangue kusoma SUA kwa
sababu tuna programu ambazo zitawapa nafasi ya kuwaandaa vizuri, mtaweza
kujiajiri ama kuajiriwa,” alisema Bi. Zahra.
Aidha, Mhadhiri huyo amewaambia wanafunzi hao kuwa programu
ambazo zinatolewa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo zinaendana na Sera ya
sasa ya Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi kuhusu uchumi wa bluu ambapo amebainisha kuwa programu kama
Shahada ya Sayansi ya Viumbe Hai na Shahada ya Sayansi ya Mazingira na
Usimamizi zina mahusiano ya moja kwa moja na uchumi wa bluu.
Bi. Mawesa Ukani, Afisa Udahili kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo akizungumza katika hadhara ya wanafunzi hao ambao ni mchanganyiko wa
masomo ya CBG na PCB amesema kupitia masomo wanayosoma ufaulu unaohitajika ili
wawe na sifa za kudahiliwa katika Chuo cha SUA ni ufaulu wa pointi 4 wa daraja
DD au CE.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kupitia baadhi ya wafanyakazi
ambao wanashiriki Maonesho ya 4 ya Elimu ya Juu Zanzibar kimeanza ziara ya
kutembelea Shule mbalimbali zinazofundisha masomo ya sayansi hapa Visiwani kwa
ajili ya kukitambulisha Chuo hicho na kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka
Zanzibar.
0 Comments